CHUO Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (CUHAS),
kimegundua kuwapo maambukizi ya bakteria mpya aina ya enterobacter
bugandesis ambao huwaathiri watoto njiti na walio na umri chini ya mwezi
mmoja.
CUHAS wanasema matibabu ya maambukizi hayo hugharimu Sh milioni 4.5.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Makamu Mkuu, Taaluma
na Utafiti wa CUHAS, Profesa Stephen Mshana, alisema bakteria hao
husababisha maambukizi ya ugonjwa (Neonatal Sepsis) ambao dalili zake ni
kupata homa kali, degedege, kupumua kwa taabu na kushindwa kunyonya.
Alisema katika utafiti wao wamebaini asilimia tano ya watoto walio
na umri chini ya mwezi mmoja ambao hutibiwa katika Hospitali ya Rufaa
Bugando (BMC) wameathiriwa na enterobacter bugandesis.
Alisema bakteria huyo husababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya dawa
kwa muda sahihi na matumizi ya dawa yasiyoidhinishwa na daktari.
Profesa Mshana alisema bakteria hao ni sugu lakini hutibika ila
matibabu yake ni ghali ambapo chupa moja ya dawa huuzwa kwa Sh 300,000
na mgonjwa huhitaji chupa 10 hadi 15 kwa matibabu ya siku saba.
“Dawa zinazotibu ugonjwa unaosababishwa na bakteria enterobacter
bugandesis ni ghali na Watanzania wengi hawawezi kumudu. Chupa moja ya
dawa inafika hadi Sh 300,000, mtoto akipatwa na tatizo hili kwa wiki
moja anaweza kuhitaji chupa 10 hadi 15,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando
(BMC), Lucy Mogele, alisema katika kipindi cha mwaka 2015 walipokea
watoto 240 walio na umri chini ya miezi miwili ambapo kati yao watoto 12
waligundulika kuwa na bakteria hao, mwaka huu tangu Januari hadi
Oktoba wamepokea watoto 180 na watoto tisa wamebainika kuwa na
maambukizi.
Akizungumzia mafanikio ya chuo hicho, Makamu Mkuu wa CUHAS, Profesa
Paschalis Rugarabamu, alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003 kimetoa
madaktari bingwa 111 kati yao wamo wa magonjwa ya akina mama, afya ya
watoto, utabibu na upasuaji ingawa idadi hiyo haikidhi mahitaji ya
taifa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment