SERIKALI imesema itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya viwanda nchini ili kuimarisha sekta hiyo.
Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru alipofunga Maonesho ya Kwanza ya Maendeleo ya Viwanda yaliyoandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) kwenye Viwanja vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Nyerere maarufu Sabasaba kwenye Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Dk Meru alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa mitaji, masoko ya uhakika na maeneo ya uwekezaji. Katika changamoto ya mitaji, alisema serikali itaanzisha Benki ya Maendeleo ya Viwanda kwa ajili ya kutoa mikopo.
“Rais alituambia tutafute maeneo ambayo nyie wazalishaji mtapeleka bidhaa zenu bila kubugudhiwa, nawahakikishia kwamba mtapata masoko ndani na pia nje ya nchi,” alisema Dk Meru.
Alisema muda umefika kwa mchango wa sekta binafsi, kutambulika rasmi na kuchangia Pato la Taifa, hivyo aliwataka Watanzania kuendeleza sekta hiyo kwa kununua bidhaa za nchini.
“Hii iwe chachu ya kujivunia bidhaa zetu, Watanzania tujenge utamaduni wa kupenda vitu vyetu, ni aibu kuona bidhaa yetu inazalishwa, lakini unataka kununua ya kutoka nchi A, Y, Z,” alisema Dk Meru.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment