WIZARA
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imesema itazifutia
usajili shule zote binafsi, ambazo zitabainika kukiuka agizo la serikali
la kuzitaka shule zote nchini kuwa na mihula miwili ya masomo badala ya
mitatu, ambayo imekuwa inafuatwa na shule zisizo za serikali.
Ili
kutekeleza azma hiyo, wizara hiyo imewaagiza wakaguzi wa shule pamoja na
maofisa elimu wa wilaya, kufanya ukaguzi katika shule binafsi zilizoko
katika meneo yao; kubaini kama kuna shule binafsi zilizokaidi kutekeleza
Waraka wa Elimu Namba Moja wa Mwaka 2015.
Kaimu Kamishna wa Elimu,
Venance Manori alisema wizara yake ilitoa waraka huo ikiwa ni njia ya
kukazia Waraka wa Serikali Namba 5 wa Mwaka 2012 ambao ulikuwa
unaelekeza mihula ya masomo kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu,
ifanane ili kuepusha usumbufu kwa walimu na kwa wanafunzi.
Waraka huo
ulifafanua kuwa kila muhula utakuwa na likizo fupi na likizo ya mwisho
wa muhula na siku za masomo kwa mwaka zitakuwa ni 194.
Pia waraka huo
unataka siku za michezo ya Umitashumita na Umiseta kwa shule za msingi
na sekondari, zifanane kwa shule zote. Lakini pamoja na kuwepo waraka
huo, baadhi ya shule zisizo za serikali zimeendelea kufuata mihula
mitatu.
Baadhi ya shule katika ripoti za wanafunzi za mwezi Desemba
kwenda kwa wazazi, wameonesha kuwa mwaka ujao wa masomo utakuwa wa
mihula mitatu na nyingine minne.
“Wizara ilifanya utafiti na
kujiridhisha kuwa haiwezekani shule zinazotoa elimu msingi kuwa na
mihula mitatu, ndio maana tukataka nchi nzima tuwe na mfumo ambao
unafanana ili kuepusha usumbufu kwa walimu na wanafunzi,” alisema
Manori.
Alisema kwanza haamini kama kuna shule ambazo sio za serikali
ambazo bado zinafuata mihula mitatu, na akaongeza kuwa kama zipo na
wizara hiyo ikapata uthibitisho, lazima hatua za sheria zichukuliwe na
hatua mojawapo ni kuzifuatia sheria.
“Ule waraka ulisambazwa kwa
mamlaka zote za utekelezaji ukiwemo umoja wa shule binafsi na taasisi
inayosimamia shule za dini ya Kikristo na shule za Baraza la Kiislamu,
hivyo hakuna kisingizio cha mtu kutopata huo waraka, hivyo lazima
wautekeleze,” alieleza Manori.
Hata hivyo, pamoja na waraka huo
baadhi ya shule binafsi, zimekaidi agizo hilo na zimeendelea kufuata
mihula mitatu, jambo ambalo ni kwenda kinyume cha maagizo hayo ya
serikali. Kutokana na ukaidi huo, Manori alisema kuanzia mwakani, shule
ambazo zitabaini kukaidi agizo hilo zitafutiliwa usajili.
Manori
alisema wakaguzi wa elimu hiyo ndio kazi yao kuhakikisha kwamba maagizo
yote ya serikali yanafuatwa. Pia alitoa mwito kwa wazazi ambao wanapata
maelekezo ya mihula ya shule inayoenda kinyume cha maagizo ya serikali,
waripoti suala hilo kwa malofisa elimu wilaya na wakaguzi wa shule.
“Sio
kwamba wazazi wote waje hapa wizarani kulalamika, wale wanaoweza walete
malalamiko hayo na walioko mikoani waende kwa maofisa elimu wa mikoa,
wilaya na wakaguzi wa shule ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,”
alifafanua Kamishna huyo.
Alisema hivi karibuni wizara yake itatoa
kalenda ya masomo na mihula, itakayofuatwa na shule zote zinazotoa elimu
msingi, kama walivyotoa kalenda ya masomo katika mwaka huu.
Pia
alikiagiza Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini
(TAMONGSCO), Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Tume ya Huduma za
Kijamii ya Kikristo ambao ndio wanasimamia shule ambazo sio za serikali
nchini, kuhakikisha wanachama wao wanatekeleza waraka huo wa serikali.
Msimamo
wa Tamongsco Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya alipoulizwa
kutoa maoni yake alisema, “Niko kwenye mkutano, lakini sisi bado
hatukubaliani na waraka huo wa serikali, nitumie e-mail yako
nitakuandikia sababu za kupinga waraka huo.”
Hata hivyo, Nkonya
baadaye alituma nakala ya barua iliyoandikwa na yeye kwenda kwa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
kumwomba shule binafsi ziendelee kutumia mihula mitatu kwa sababu
inarahisisha ukusanyaji wa ada kutoka kwa wazazi na walezi.
Nkonya
pia alisema Tamongsco imetaka mihula mitatu kwa sababu mfumo huo
unaruhusu baadhi ya shule kufungwa Aprili wakati huo ambao huwa na mvua
za masika katika baadhi ya sehemu nchini, mvua inaharibu barabara na
hivyo kusababisha gharama kuongezeka kutokana na magari ya shule
kuharibika.
Alisema Tamongsco pia imebaini kuwa mihula hiyo mitatu, inatoa fursa kwa wenye shule kuzifanyia matengenezo shule zao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment