Image
Image

Rais Magufuli awaalika viongozi wa Afrika kutembelea Tanzania.

RAIS John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na marais watatu wa nchi za Afrika, Waziri Mkuu wa Ethiopia na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kando ya Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) uliomalizika mjini Addis Ababa, Ethiopia, jana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli amewaalika viongozi wote kuitembelea Tanzania ili wapate muda zaidi wa mazungumzo ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwa lengo kukuza zaidi biashara, uwekezaji na kuboresha maisha ya wananchi.
Alikutana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambapo viongozi hao wamezungumzia miradi mbalimbali ya ushirikiano na fursa za biashara ambazo Tanzania na Uganda zinaweza kuzitumia kujiongezea mapato. Rais Museveni amekubali kufanya ziara nchini katika siku za karibuni.
Aidha, Rais Magufuli amekutana na Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi ambapo viongozi hao wamezungumzia namna nchi hizo zitakavyoshirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo na viwanda.
Pamoja na kukubali mwaliko wa Rais Magufuli wa kufanya ziara rasmi nchini, El-Sisi pia amekubali ombi la kuwaleta wataalamu na wawekezaji wa Misri nchini ili wajenge viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba vya binadamu, kuinua teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji, kuwekeza katika viwanda vya nyama na viwanda vingine ambavyo nchi hiyo imepiga hatua kubwa.
“Mheshimiwa Rais El-Sisi nakupongeza sana kwa juhudi zako za kuijenga Misri na nitafurahi sana kuona biashara ya Tanzania na Misri inaongezeka maradufu kwa manufaa ya pande zote mbili,” alisisitiza Dk Magufuli.
Jana, pia Rais Magufuli alikutana na Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ambaye pamoja na kukubali kufanya ziara rasmi nchini, viongozi hao wamekubaliana kuwa baada ya kazi kubwa ya harakati za ukombozi nchi hizi sasa zina kila sababu ya kuelekeza nguvu katika kuongeza biashara na uwekezeji.
Mbali na marais hao, Dk Magufuli amekutana na Rais wa AfDB, Akinwumi Adesina ambaye pamoja na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri ambao Tanzania inaupata kutoka benki hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, amemuomba kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano huo hasa katika maeneo ya kipaumbele ambayo Tanzania inayatekeleza hivi sasa.
Adesina amesema benki hiyo itaendeleza ushirikiano na uhusiano wake na Tanzania na kwamba Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele vipya vya AfDB viitwavyo “Hi 5” vinavyohusisha uwezeshaji miradi ya uzalishaji wa nishati, ujenzi wa viwanda, uzalishaji wa chakula, miundombinu ya kuunganisha nchi na nchi na kuboresha maisha ya watu.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment