Hatua hiyo ya gazeti hilo linalomilikiwa na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd ilichukuliwa jana baada ya juzi kupewa saa 24 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo, Dk Hassan Abbasi kuomba radhi kutokana na taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo katika toleo la juzi Januari 30 hadi Februari 5, mwaka huu likibeba kichwa cha habari “Ufisadi ndani ya ofisi ya JPM.”
Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Maelezo jana, Mhariri wa gazeti hilo, Jabir Idrissa anakiri kuwa habari hiyo haikuleta taswira nzuri kwa Rais Magufuli na umma, kwani imehusu Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na siyo Ikulu.
“Ninakiri kwamba habari hii haikuleta taswira nzuri kwa Mhe. Rais na hata umma kwani imehusu Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na siyo Ikulu. Ni kweli kabisa kwamba hakuna mazingira yoyote yanaweza kuhalalisha kumhusisha Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika habari hii.
“Kutokana na hali hiyo, nachukua nafasi hii KUMUOMBA RADHI Mhe. Rais, Serikali anayoiongoza pamoja na umma wa Watanzania kwa dhana isiyopendeza iliyojengeka kutokana na habari tuliyochapisha. Ninaahidi kuwa katika utendaji wetu wa kazi, tutakuwa waangalifu zaidi,” ilisema barua ya Mhariri wa MwanaHALISI.
Katika taarifa yake juzi, Mkurugenzi wa Maelezo alisema licha ya habari hiyo kujenga dhana kuwa Rais Magufuli anahusika na kilichoitwa ufisadi, msingi wa taarifa husika ni tatizo la manunuzi katika Shirika la Elimu Kibaha!
“Kwa kuwa ni jambo lililo dhahiri kuwa Shirika la Elimu Kibaha si ofisi, idara wala kitengo “ndani ya ofisi ya JPM” mwandishi na mhariri wa habari husika wamedhihirisha malengo ya kumchafua Rais binafsi kwa jamii.
“Aidha, katika siku za karibuni Serikali imejitahidi kufanya mazungumzo na wahariri wa gazeti hili kwa lengo la kukumbushana maadili ya uandishi wa habari, ni bahati mbaya kwamba wamekuwa wakikaidi japo wito tu.
“Kwa sababu hizi, serikali inawaagiza wahariri wa gazeti hilo kujitathmini na kuchukua hatua kwa kutumia kifungu cha 40 cha Sheria ya Huduma za Habari, 2016 kinachowapa fursa ya kuomba radhi, kwa kumuomba radhi Rais ndani ya saa 24 kuanzia saa 10 jioni ya leo Januari 30, 2017,” alieleza.
0 comments:
Post a Comment