Image
Image

Serikali yazindua kifaa cha kubaini Selimundu ndani ya dakika 5.

SERIKALI imezindua kifaa kipya cha kugundua ugonjwa wa selimundu, ambacho kitatoa majibu ndani ya dakika tano na kueleza kuwa kitaongeza nafasi za kuishi kwa wagonjwa hao kwa asilimia 50 kutoka asilimia 20 ya sasa.
Aidha, kifaa hicho kina uwezo wa kufanya kazi kwenye mazingira yasiyo na umeme na kwamba kitaweza kutumika katika vituo vya afya ili kuwagundua wagonjwa hao mapema.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangwala wakati wa uzinduzi wa kifaa hicho kilichotolewa na Kampuni ya Medomix.
Dk Kigwangala alisema kifaa hicho kitaboresha huduma za uchunguzi na matibabu kwa tatizo la selimundu na kuongeza uelewa kwa jamii juu ya tatizo hilo. Alisema kifaa hicho kinaweza kugundua aina mbalimbali za selimundu kwa wagonjwa kwa teknolojia rahisi isiyohitaji matumizi ya umeme wala wataalamu waliobobea.
“Kampuni hii imeanza kupanua huduma zake kwa kuagiza vifaa na vitendanishi vya kutosha ili vitumike nchini. Mategemeo yangu kifaa hiki kitatumiwa na kutoa majibu yenye ubora na hivyo kuongeza ufanisi katika kutoa tiba sahihi kwa wagonjwa watakaogundulika,’’ alisema Dk Kigwangala.
Alifafanua kuwa kifaa hicho kimepata usajili baada ya kupitia hatua za usajili nchini ikiwemo kusajiliwa na bodi ya maabara binafsi za afya.
Alisema kuwa kitendo cha Kampuni ya Medomix cha kuagiza kitendanishi cha kupima selimundu imekuja kwa wakati sahihi ambapo nchi imekuwa na wagonjwa wengi wanaopatiwa matibabu nje ya vituo vya afya na hivyo kufanya gharama kuwa kubwa.
“Naamini kuwa kampuni nyingine zitaunga mkono kwa kuendeleza utaratibu huu ili huduma nyingine ziweze kutolewa kwenye vituo vya afya wilayani na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa hospitali za Rufaa za Mikoa au zile za Kanda kwa ajili ya vipimo na matibabu,’’ alieleza.
Kwa mujibu wa Dk Kigwangala, serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi; mikakati hiyo ni pamoja na kutengeneza mpango mkakati wa kitaifa wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo selimundu.
Pia alisema wanatoa elimu ya umma juu ya tatizo hilo, kutoa huduma za upimaji na ugunduzi wa seli mundu, upimaji wa matatizo yanayoambatana nayo na upimaji wa selimundu kwa watoto wachanga wanaozaliwa ili kuwatambua mapema pamoja na kutoa huduma za tiba na kinga kutolea huduma.
“Takwimu zinaonesha kuwa watoto wapatao 321,307 huzaliwa na tatizo la selimundu kila mwaka. Asilimia 76 ya watoto hawa huzaliwa Afrika sawa na watoto 237,253 kila mwaka,’’alisema na kuongeza; “Kwa hapa Tanzania kati ya watoto 8,000 hadi 11,000 huzaliwa na tatizo hilo na kati ya watoto hawa asilimia 15 hadi 18 ni wenye dalili za ugonjwa huo.’’
Kwa upande wake, Mratibu wa Idara ya Magonjwa ya Damu, Kitengo cha Selimundu kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), Dk Deogratius Soka, alisema kuwa changamoto kubwa wanazokabiliana nazo ni uelewa mdogo wa watu kuhusu ugonjwa huo na kwamba lengo lao ni kuwaelimisha wajitokeze kupima afya zao.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment