SIMBA na Yanga leo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mwaka huu, safari hii zikikutana nje ya Uwanja wa Taifa na si kwenye mechi ya Ligi Kuu bara bali Kombe la Mapinduzi.
Watani hao wa jadi wanakutana kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, ikiwa ni mara ya tano sasa kukutana kwenye uwanja huo baada ya kukutana mwaka 1975 kwenye mechi ya fainali ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame) ambapo Yanga ilishinda mabao 2-0.
Mara ya pili miamba hiyo ilikutana mwaka 1992 kwenye fainali za michuano hiyohiyo na Simba kushinda kwa mikwaju ya penalti 6-5 kabla ya kukutana tena kwenye fainali za kombe la Muungano mwaka huohuo na Simba kushinda kwa bao 1-0 na mara ya mwisho zilikutana mwaka 2011 kwenye fainali za Kombe la Mapinduzi na Simba ilishinda mabao 2-0.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ni Oktoba mosi mwaka jana kwenye mechi ya Ligi Kuu na kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi iliyotawaliwa na vurugu zilizosababisha serikali kuzifungia kutumia Uwanja wa Taifa baada ya mashabiki kuharibu miundo mbinu.
Simba inaingia katika mechi hiyo ikitoka kuwa kinara wa kundi B baada ya kushinda mechi zake tatu na kuifanya ifikishe pointi 10.
Yanga wanaingia nusu fainali ya leo wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 4-0 na Azam katika mechi ya mwisho ya makundi iliyochezwa Jumamosi iliyopita.
Ubingwa wa Mapinduzi Rekodi zinaonesha kuwa Simba ndio timu inayoongoza kulitwaa taji hilo mara nyingi zaidi ikiwa imetwaa mara tatu wakati watani wao Yanga wamewahi kulitwaa mara moja pekee tangu kuanzishwa kwake, huu ukiwa ni mwaka wa 10.
Azam ni timu ya pili kwenye rekodi hiyo ikiwa imelitwaa mara mbili. Mbali na rekodi hiyo, pia Simba inaongoza kucheza mechi za fainali ya michuano hiyo ikiwa imecheza mara tano wakati watani wao wamecheza mara tatu pekee. Akizungumzia mchezo wa leo, Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema:
“Tumekaa na wachezaji wetu na kuzungumza nao, hatutegemei tena kupoteza mchezo wetu baada ya ule wa Azam, benchi la ufundi tumejua makosa yetu, na wachezaji wana makosa yao, hayo yameshapita kwa kifupi tumejiandaa vema na mchezo huo”.
Wakati Mwambusi akisema hayo, winga wa klabu hiyo Simon Msuva ambaye amewaomba radhi mashabiki wao kwa kipigo cha Azam, alisema watahakikisha wanatoka na ushindi katika mchezo wa leo.
“Mpira ni mchezo wa makosa, ya Azam yalishapita, sasa tunaganga yajayo, hatutakubali kupoteza mchezo wetu na Simba, tunajua ni mchezo mgumu lakini mimi na wachezaji wenzangu tutajitahidi tuwape raha mashabiki wetu,” alisema Msuva.
Kwa upande wa kocha msaidizi wa klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi, Jackson Mayanja alisema:
“Sisi tumekuja kushinda, kila mechi kwetu ni fainali, Yanga ni timu nzuri, ni mahasimu wetu tunawaheshimu, tumejipanga kutoka na ushindi,”alisema.
Kwa upande wa nahodha wa Simba, Jonas Mkude alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu kila timu imejiandaa vizuri lakini hawana wasiwasi na mchezo huo.
“Sisi tumejiandaa vizuri, ni matumaini yetu na wao wamejiandaa vizuri, mchezo wa mpira wa miguu ni maandalizi, baada ya maandalizi tutakutana tutacheza, utakuwa mchezo mzuri, kipimo kizuri kwetu na kwao, dakika 90 zitaamua,”alisema.
Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 2:15 usiku na kabla ya hapo itatanguliwa na nusu fainali nyingine kati ya Azam na Taifa Jang’ombe saa 10 jioni.
Mechi hiyo pia inatarajiwa kuwa na upinzani wa juu hasa kwa vile Jang’ombe imetoka kumfunga bingwa mtetezi, URA na Azam imetoka kuifunga Yanga mabao 4-0 katika mechi za mwisho za makundi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo Khamis Said alisema kuwa michezo yote miwili ya nusu fainali viingilio vyake havitabadilika na badala yake vitakuwa ni vile vile ambavyo vinatumika toka kuanza kwa mashindano hayo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment