Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza zaidi ya majina ya wanafunzi 8,436 kutoka vyuo vya elimu ya juu 52 nchini wasiokuwa na sifa ya kufanya masomo ya ngazi hiyo.
Sehemu ya taarifa kwa umma ambayo imewekwa kwenye tovuti ya tume hiyo imesema, "TCU inautangazia umma kuwa zoezi la uhakiki wa sifa za wanafunzi wanaondelea na masomo kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mwaka 2016/2017 limekamilika katika baadhi ya vyuo," liliandika tangazo hilo.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, majina ya wanafunzi hao wasiokuwa na sifa, wamo hadi waliopo mwaka wa mwisho wa masomo yao.
Taarifa hiyo iliyotolewa Februari 20 na kuwekwa kwenye tovuti ya tume hiyo inasema.
"Katika kutekeleza zoezi hilo tume imebaini kuwa kuna wanafunzi ambao wamedahiliwa katika program ambazo hawana sifa. Orodha ya wanafunzi wasio na sifa imeshawasilishwa kwenye vyuo husika," inasema sehemu ya taarifa hiyo.
"Tume inawaarifu wanafunzi wote ambao majina yao yame orodheshwa wawasiliane na vyuo vyao ili kuthibitisha sifa zao kabla ya Februari 28, ambao hawatafanya hivyo hawatatambuliwa na Tume na hivyo kukosa sifa za uanafunzi," ilisema.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa TCU, Edward Mkaku, alisema pamoja na mambo mengine uhakiki huo ulifanywa kwa kuangalia taarifa za wanafunzi hao zilizopo kwao na kuzilinganisha na zile za Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).
Alisema katika kulinganisha taarifa hizo, walibaini kwamba kuna utofauti kati ya taarifa zilizopo kwao na zile zilizopo Necta, hivyo wameamua kutoa muda kwa wanafunzi wote wawasilishe taarifa ambazo wanadhani ni sahihi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizo kwenye tovuti ya TCU, baadhi ya vyuo na idadi ya wanafunzi wasiokua na sifa ni Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dodoma, chenye wanafunzi 375, CBE Mwanza, 101, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) 301, Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) 149, Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) 96 , CHUO Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM) 162, Huku Chuo Kikuu cha Mzumbe kikiwa na wanafunzi 639.
Vingine ni Chuo Cha Mtakatifu Agustino (SAUT) wanafunzi 1,046, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana (SJUT) 968, Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) 164, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) 966, Chuo Kikuu cha Sumait Zanzibar 552, Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TURDACO) 74, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) 52, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) 224, Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) 522.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment