Image
Image

Zifahamu faida zitokanazo na rasilimali za bonde la mto nile kwa Tanzania.

Mto Nile ni miongoni mwa mito mikubwa iliyopo upande wa Mashariki ya Bara la Afrika na Duniani kote ukiwa na urefu wa kilomita 6,695 ambapo beseni ya Nile hukusanya maji ya eneo linalojumuisha 10% za eneo la Afrika yote.
Kwa muonekano wa juu Mto Nile unaonekana kama pembetatu wakati upande wa chini wa eneo la Nile (Kaskazini) na upande wa juu (Kusini) kuna mimea mbalimbali inayoota kwa wingi pia katika kipindi cha mwisho wa mwaka eneo la mto Nile huwa linakuwa na mwonekano mwekundu na kuwa na maua yanayojulikana kama lotus flowers.
Japokuwa mimea hii haioti kwa wingi wakati huu kama ilivyokuwa hapo awali, mimea inayoota kwa wingi katika eneo la Mto Nile kwa upande wa chini ni yale yanayojulikana kama Egyptian lotus na kwa upande wa juu hujawa na mimea inayoitwa Cyperus papyrus.
Chemchemi za Nile ni mito yote inayopeleka maji kwenda Ziwa Viktoria katika nchi za Tanzania, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Kenya na kwa upande mwingine wa Nile unaanzia Ethiopia ukiitwa Abbai au Nile ya Buluu unatoka katika Ziwa Tana wakati chanzo cha mbali kabisa ni mto wa Luvironza huko Burundi unaoingia katika mto wa Kagera na kufika Ziwa Viktoria.
Mto huo ambao unaanzia Ziwa Victoria nchini Tanzania, ni chanzo  kikubwa cha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani, kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha umeme kwa wakazi wa nchi za bonde hilo.
Kutokana na nchi nyingi kuzungukwa na mto Nile, suala la ushirikiano katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto huo limepewa kipaumbele ili kuzuia migogoro inayoweza kuzuka baina ya nchi ambazo wanatumia mto huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent Ntabana anasema kuwa azma ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile limepewa kipaumbele na nchi zote zinazozungukwa na mto huo, jambo hilo ndilo limesababisha kuanzishwa kwa Sekretarieti ya NBI mwaka 1999 jijini Dar es Salaam.
“NBI ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile kwa niaba ya nchi wanachama zipatazo 10 ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Misri,” anasema Ntabana.
Kwa upande wa Mratibu wa Kanda wa Kitengo cha Uratibu cha Bonde la Mto Nile (NELSAP-CU), Elicad Nyabeeya anasema kuwa mto huo una manufaa makubwa kwa nchi wanachama kwani muunganiko wa nchi hizo umeleta mawasiliano mazuri ambayo yanapelekea kuinua uchumi wa nchi hizo pia kwa upande mwingine uwepo wa ushirikiano huo umesaidia nchi wanachama kufahamu tamaduni za watu tofauti tofauti.
Nyabeeya anakaririwa akisema kuwa “Nchi ya Tanzania inafaidika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na NBI kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa bwawa la Bisrawi na usanifu wa bwawa la Borenga, mkoani Mara”.
Kwa mujibu wa Nyabeeya, nchi hii itanufaika na miradi ya maji na nishati ya umeme, pamoja na miradi mingine mingi ambayo NBI inaendelea kuitekeleza kama vile ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na umwagiliaji katika mabonde ya mito Kagera na Ngono iliyopo mkoani Kagera.
Anaendelea kufafanua kuwa mradi wa umeme wa Rusumo utazalisha megawati 80 za umeme ambazo zitatumiwa na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo Tanzania inatarajiwa kupata megawati 16.
Miradi mingine ni ya kuunganisha umeme kutoka Ethiopia, Kenya hadi Tanzania, mradi wa umeme kati ya Tanzania na Zambia.
Aidha, NBI wanatarajia kukamilisha upembuzi yakinifu wa kina wa miradi ya Mara na Ngono ifikapo mwezi Aprili mwaka huu ambapo wananchi 20,000 pamoja na hekari 13,630 katika vijiji 21 vinatarajiwa kunufaika na mradi wa Ngono wakati Bonde la Mara litanufaisha wanachi 10,000. Miradi hiyo itahusisha usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, mifugo na shughuli za umwagiliaji.
Wakati huo, Bwawa la Borenga litakuwa likisambaza maji katika Bonde la Mara kwa wakazi wa vijiji 13 kwa ajili ya umwagiliaji na 17 vitapata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na mifugo.
Madhumuni ya miradi hiyo ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji ya uhakika, kuimarishwa kwa soko na mahusiano na kukuza sekta binafsi, kilimo, usalama wa chakula na kupunguza umaskini.
Kutokana na kuwepo kwa umuhimu wa rasilimali za Bonde la mto huo, iliamuliwa kuwa Februari 22 ya kila mwaka iwe ni siku rasmi ya kuadhimisha uanzishwaji wa muunganiko wa matumizi ya pamoja ya rasilimali za mto huo baina ya nchi 10 wanachama .
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Sylvester Matemu amesema kuwa lengo la Siku ya Nile ni kukuza uelewa kwa watu wote kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zote wanachama, masuala yanayotekelezwa na faida inayopatikana kutokana na matumizi bora ya rasilimali za Bonde la Mto huo.  
“Maadhimisho ya siku ya Nile kuadhimishwa katika nchi fulani ni tukio la kihistoria kwasababu ni tukio ambalo halifanyiki katika nchi moja kila mwaka hivyo kwa vile nchi wanachama tuko 10 basi  linatokea mara moja kila baada miaka 10,”anasema Mhandisi Matemu.
Maadhimisho ya 11 ya Siku ya Nile kwa mwaka huu yameadhimishwa nchini Tanzania kwa ushirikiano wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na Sekretariati ya Nile Basin Initiative (NBI) ambapo mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 600 wakiwemo Mawaziri wa nchi wanachama kutoka kwenye nchi husika, mabalozi mbalimbali, wabunge, watu kutoka taasisi na mashirika mbalimbali pamoja na wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu.
Shughuli hizo zilianza kwa maandamano yaliyoongozwa na Bendi ya Polisi kuanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambako maonesho pamoja na ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo vilifanyika.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment