WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imepokea vifaa vya maabara ya masomo ya Fizikia, Kemia na Baolojia vyenye thamani ya Sh bilioni 16.9 kwa ajili ya shule za sekondari nchini.
Vifaa hivyo vimetolewa na Kampuni ya Lab Equip Ltd ambayo ni miongoni mwa wazabuni watano walioshinda kusambaza vifaa hivyo kwa kanda 11 ambazo ni Kanda ya Kaskazini Mashariki na Kanda ya Kaskazini Magharibi.
Nyingine ni Kanda za Magharibi, Kati, Kusini, Ziwa, Nyanda za Juu, Dar es Salaam, Mashariki, Ziwa Magharibi na Nyanda za Juu Kusini.
Akipokea msaada huo Dar es Salaam, Kaimu Kamishna wa Elimu wizarani hapo, Nicolas Buretta alisema vifaa hivyo vitasambazwa kwa shule za sekondari 1,696 nchini, kati ya hizo, shule 1,625 ni za kata na shule 71 ni shule kongwe za Serikali.
Alisema vitasambazwa katika shule zilizokamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara na kwamba, hiyo ni changamoto kwa shule ambazo hazijakamilisha majengo yao ili zikamilishe.
Kaimu Kamishna huyo alisema vifaa hivyo vitasambazwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), na kwamba kazi hiyo ya usambazaji itakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
“Vifaa hivi vitaleta matokeo chanya katika masomo ya sayansi. Ujifunzaji wa vitendo utainua ari kwa wanafunzi katika kujifunza. Italifanya taifa kuwa na wataalam wa kutosha kwa kuwa hatutakuwa na changamoto ya vifaa,” alisema.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni ya Lab Equip Ltd, Hassan Raza aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na timu yake kwa kuwaamini.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment