Image
Image

Maalim Seif:Ni bora nikae na CCM adui, kuliko kukaa na Lipumba Msaliti.



Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kamwe hatamsamehe wala kukaa meza moja na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kutokana na hali hiyo amesema ni bora akae meza moja na kiongozi yeyote wa CCM lakini si Profesa Lipumba kwa sababu ni msaliti.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya awamu ya kwanza, alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Kituo cha Clouds TV.
“Siwezi kukaa meza moja na Lipumba na siwezi kumsamehe kwa jinsi alivyotusaliti. Ni bora nikae na CCM adui kwani ninawajua kabisa ni adui lakini si msaliti Lipumba…siwezi kukaa na msaliti kamwe,” alisisitiza.
Alipoulizwa kuwa yeye kama kiongozi anapaswa kusamehe kwa sababu hata vitabu vya dini vimeeleza hivyo alisema. “Kwa Lipumba alivyotusaliti no…no way siwezi kumsamehe. Kwanza haji kujenga CUF bali kuibomoa kwa fedha alizopewa,” alisema.
Akaulizwa tena mbona huko nyuma aliwahi kuwa na uhasama wa wazi na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na baadaye akakaa meza moja na Ukawa?
Alisema. “Uhasama wangu na Sumaye ulikuwa tofauti za kichama na nilimjua wazi kuwa ni adui kwa sababu alikuwa CCM lakini kwa Lipumba ni tofauti kwani ni msaliti,” alisema.
Akizungumzia kuhusu kukataa kumpa mkono Rais Dk. Mohamed Ali Shein walipokutana katika mazishi ya Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, alisema alifanya makusudi kwa sababu alipora haki yake.
 “Huyu Shein (Rais wa Zanzibar) ndiye aliyepora haki yangu, leo wananchi waone namchekea watanitafsiri vipi mimi…nilikataa kumpa mkono kwa makusudi ili na yeye afeel (atafakari)  kwa uporaji alioufanya aseme kumbe mwenzangu huyu hakuridhika,” alisema.
Akifafanua kuhusu kauli ya Rais Dk. John Magufuli,  kwamba ingekuwa yeye amenyimwa mkono asingetoa fedha zozote hata za matibabu, Maalim Seif alisema mkuu huyo wa nchi alipotoshwa.
Maalim Seif ambaye alipata kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alisema tangu aondoke katika wadhifa huo, ziara zote alizokuwa akizifanya nje ya nchi pamoja na matibabu, alikuwa akijihudumia mwenyewe.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Maalim Seif alishindana na Dk. Shein ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, 2016.
Akizungumzia kuhusu chama hicho kwamba kinaendeshwa kwa fedha gani baada ya ruzuku kuzuiwa, alisema hivi sasa chama hicho kinaendeshwa kwa fedha za wanachama.
“Tuliwaambia wanachama kwamba tulikuwa na ruzuku lakini sasa hatuna, baadaye wakasema lazima wachange wenyewe. Hivyo sasa tumeweka utaratibu kwamba ukiwa kiongozi wa taifa unachangia Sh 10,000 kila mwezi, kiongozi wa wilaya unachangia Sh 3000 kila mwezi, kiongozi wa jimbo unachangia Sh 2000 kila mwezi na mwanachama wa kawaida anachangia Sh 1000,”alisema.
Utendaji wa Magufuli
Alizungumzia pia utendaji wa Rais Magufuli, akisema kuna mambo ambayo amefanya vizuri lakini kitendo cha kutowachukulia hatua baadhi ya watu inamwondolea sifa hiyo ya utendaji mzuri.
“Kuna mambo ambayo amefanya vizuri na mengine kwa mawazo yangu kwa kweli kuna kasoro nyingi, kubwa pamoja na kwamba anaonekana mpigania haki, asiyependa rushwa, ubadhirifu, lakini vilevile kuna watu ambao hata akifanya nini hao hawaguswi sasa huwezi ukawa kiongozi ukiwa na double standard,”alisema.
Akizungumzia kuhusu uhuru wa habari, alisema hivi sasa hakuna uhuru wa habari huku akiishauri Serikali kuacha kuwabana waandishi wa habari na kwamba pale wanapoona amekosea afikishwe mahakamani.
Alipoulizwa akiwa Dar es Salaam iwapo anakwenda katika ofisi za chama hicho Buguruni, alisema. “Pale hivi sasa kuna maharamia ndiyo tatizo moja tunalo hilo, tunafanya mikutano yetu hotelini.  
“Vijana wanataka wakaikomboe ofisi yao lakini nimewaambia watulie, tunatafuta haki kwa njia za amani muda si mrefu, nina matumaini makubwa kabisa inshallah haki itarudi,” alisema. 
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment