SERIKALI imewaonya watumishi wa umma waliotajwa kuhusika na kughushi vyeti wapatao 9,932 kwamba wasifanye mzaha na suala hilo na kwamba wanaokusudia kukata rufaa, ikibainika wameendelea kuidanganya serikali, watapata adhabu kubwa zaidi.
Aidha, imebainika kwamba wapo watu wanaopata mamilioni kwa kuwahadaa walioingia kwenye orodha ya watumishi wenye vyeti feki kwa kutoa kati ya Sh milioni moja hadi Sh milioni nne ili kuondolewa katika orodha hiyo. Kwa nyakati tofauti jana mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Laurean Ndumbaro, wametoa kauli za kuonya kuhusu watumishi hao wenye vyeti feki kuwa wasifanye mzaha na suala hilo.
Akijibu mwongozo bungeni jana, Kairuki alisema wote wenye malalamiko halali waandike barua kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kupitia kwa waajiri wao kulalamika. Alisema wanaolalamika kuwa wameonewa huku wanajua kwa uhakika kwamba walighushi vyeti vyao, ikibainika wameendelea kuidanganya serikali watapata adhabu kubwa. Kairuki alisema taarifa ya uhakiki ilivyotoka Aprili 28, mwaka huu wapo ambao wamekubali na kuachia ofisi kabla ya Mei 15, mwaka huu ambayo ni siku ya mwisho na wengine wanapinga kwamba hawana vyeti feki.
“Wale wote ambao wameghushi vyeti wanatakiwa kujiondoa kwenye ofisi zao kabla ya Mei 15, mwaka huu, na kwa wanaopinga ikiisha tarehe hiyo kama hujakata rufaa, unatakiwa wasiwepo kazini,” alieleza Waziri Kairuki ambaye Ijumaa iliyopita, alikabidhi orodha ya uhakiki wa watumishi wa umma kwa Rais John Magufuli. Alisema kwa wale wanaotaka kulalamika wanatakiwa kuandika barua Necta kupitia kwa waajiri wao ambaye ataunganisha nakala vya vyeti na baadaye zitapelekwa kwa Katibu Mkuu Utumishi kwa uhakiki wa utumishi wake. Alisisitiza kuwa wafanyakazi ambao wanajua wameghushi vyeti vyao, wasifanye mzaha na suala hilo, ikitokea kwamba mtumishi huyo anasumbua serikali, basi adhabu itakayokuwa itakuwa kubwa sana.
Kwa hao, ambao watakuwa wamekata rufaa, uhakiki utafanyika kwa umakini zaidi. Mapema bungeni, Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (CCM) aliomba mwongozo akisema baadhi ya watu wamelazwa hospitalini kutokana na kutajwa kwenye orodha ya watu wenye vyeti feki. Rwamlaza alisema wafanyakazi wanne wamepata shinikizo la damu na kulazwa hospitalini baada ya kusikia ripoti ya Rais ya watumishi walioghushi vyeti.
“Wengine walikuwa wakikaribia kustaafu na wengine walikuwa masomoni na wengine hawajasoma sekondari wakati huo. Serikali inaonekana haijahakiki vizuri watu ambao wameghushi vyeti badala yake imewaingiza watu ambao hawahusiki,” alidai mbunge huyo. Kwa upande wake, Katibu Mkuu Dk Ndumbaro akizungumza na waandishi wenye Ukumbi wa Habari Bungeni Dodoma, alisema wanaotaka kukata rufaa wafanye hivyo kabla ya Mei 15, mwaka huu.
Alisema wanaolalamika watatakiwa kuwa na vyeti halisi ambavyo watavipeleka kwa mwajiri ambaye ataviskani na kupeleka nakala zake na nakala laini (soft copy) kwa Necta pamoja na barua ya kuthibitisha vyeti hivyo ambao watazipeleka kwa Katibu Mkuu Utumishi. “Wanasema wameonewa wana vyeti halali, wakate rufaa kwa kuandika barua kupitia kwa waajiri wao ambapo watathibitisha na kuambatanisha nakala za vyeti ambavyo vitaskaniwa na kupelekwa nakala ngumu na nakala laini Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na kutoka kwapo zitakwenda kwa Katibu wa Mkuu Utumishi,” alifafanua.
Dk Ndumbaro alisema vyeti hivyo wanaangalia index namba na gamba la vyeti vyenyewe, nakala hizo za vyeti vilivyoskaniwa au nakala laini, zinaweza kutumwa kwa njia ya barua pepe ya Necta na wizara kabla ya Mei 15, mwaka huu. Alisema uhakiki ambao ripoti yake iliwasilishwa kwa Rais, Aprili 28, mwaka huu, ulihusisha vyeti vya kidato cha nne na sita na vyeti vya ualimu kwa watumishi wa Serikali za Mitaa, taasisi za umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Alisema uhakiki wa taasisi za umma zilizobaki zikiwamo wizara mbalimbali, ukiachilia mbali ya Utumishi utatolewa Mei 10, mwaka huu.
Katika uhakiki huo uliopita, alisema au huu unaotolewa Mei 10, hauhusishi wanasiasa kutokana na mfumo wa ajira yao, wakiwa wakuu wa mikoa, wabunge, wakuu wa wilaya, rais, makamu wa rais na waziri mkuu. Dk Ndumbaro alisema kati ya wafanyakazi 9,932 wanaondolewa mishahara ya mwezi huu wa tano, mwishoni mwa mwezi huu hawatapata mishahara, lakini watakaokata rufaa na kubainika kwamba wana vyeti halali, watalipwa mishahara yao.
Alisema kwa wafanyakazi 1,538 wenye vyeti vyenye utata ambavyo inaonekana vinatumika na watu wawili au watatu au zaidi, wanatakiwa kwenda kuhakiki vyeti vyao Necta ili ionekane nani mwenye vyeti halali na nani walighushi. “Lakini kwa sasa kabla ya kuthibitisha yupo mwenye cheti halali, watasimamishwa mishahara yao hadi hapo Necta itakapohakikisha kwamba mtumishi yupo ni halali, mmiliki wa cheti hicho, ndiye atakayepata mshahara,” alieleza Katibu Mkuu Utumishi.
Dk Ndumbaro alisema wafanyakazi 11,596 waliowasilisha vyeti pungufu, wanatakiwa kukamilisha vyeti vyao kabla ya Mei 15, mwaka huu, wasipofanya hivyo baada ya tarehe hiyo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa. Katibu Mkuu huyo alisema wamebaini kwamba wengi wa wanaolalamika ni wale ambao walikuwa wakitumia vyeti tofauti zaidi na kile cha daraja la nne ambalo hawakufanyia kazi, lakini sasa wanaleta vyeti vya daraja la tatu, hao nao wameghushi vyeti kutokana na kwamba wanatumia vyeti vya daraja la tatu walivyokuwa wameghushi.
Aidha, amesema kutokana na mkakati wa kuondoa wafanyakazi wenye vyeti feki, zipo kada, idara, taasisi na maeneo ambayo yameathirika kwa kuondokewa na wafanyakazi wengi, wahusika wanatakiwa kupeleka maombi katika Ofisi ya Utumishi haraka. Alisema viongozi au wasimamizi wa maeneo hayo, wanatakiwa kupeleka maombi haraka ili ofisi yake itoe kibali cha ajira cha dharura kuziba mapengo hayo yaliyopo. “Katika maeneo hayo vibali vitakapotolewa wasimamizi hao wanatakiwa kuzingatia sifa bora za waombaji kwamba lazima wawe waombaji wenye vyeti halali vilivyoidhinishwa na vyuo walivyosoma,” alieleza mtendaji huyo wa Utumishi.
Kuhusu wajasiriamali wanaopata fedha mamilioni kwa kuwahadaa walioingia kwenye orodha ya watumishi wenye vyeti feki, Dk Ndumbaro alisema wasidanganyike hakuna uwezekano wa kuondolewa majina hayo na mtu kwenye orodha hiyo. Alieleza kuwa mfumo ulivyo sasa ni vigumu mtu kuondolewa kwenye orodha ya watumishi waliokuwa na vyeti feki, wakitoa fedha hizo wanajisumbua bure.
Alisema wapo wajasiriamali wanaodanganya kwamba wao ni watumishi katika Baraza la Mitihani au Ofisi ya Rais Utumishi na kwamba watoe kuanzia Sh milioni moja hadi nne ili waondolewe kwenye orodha hiyo, wanajidanganya, hakuna uwezekano huo. Alisema watu hao wanafanya dili la watu kula fedha za watu walioingizwa kwenye orodha ya watu wenye vyeti feki wala hakuna uwezekano wa mtu kuondolewa kwa kuhonga au kutoa fedha, haiwezekani kabisa. Kuhusu hatima ya mafao yao kwa sababu walikuwa wakichangia kuwenye mifuko ya jamii, Dk Ndumbaro alisema wanaendelea kuangalia sheria na kuwasiliana na mifuko hiyo watatoa taarifa baadaye.
Home
News
Slider
Kairuki awaonya wenye veti feki wanaotaka kukata rufaa, asema wasifanye mzaha na suala hilo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment