Kauli hiyo imekuja kufuatia kukamatwa kwa mwanafunzi wa uuguzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amesema kuwa, jeshi hilo halitaacha kuwachukulia hatua, wote wanaojihusisha na dawa hizo. “Tutashirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama, tutawafuatilia wanafunzi na wasambazaji, popote walipo hawatakuwa salama,” alisema.
Aliwataka wanafunzi kuzingatia masomo na si kujiingiza kwenye biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Kamanda Mambosasa aliwataka wanafunzi wenye taarifa za wanaofanya biashara hiyo au kutumia dawa hizo kutoa taarifa ili waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Mwanafunzi kaenda shuleni kusoma lakini anauza bangi ili aharibu akili za wenzake, tunaendelea kuwabaini wanaojihusisha na usambazaji na utumiaji dawa za kulevya,” alisema.
Alisema jeshi hilo halitaacha kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na biashara hiyo. Mei 9 mwaka huu, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa kozi ya Uuguzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nelson Matee (24) alikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa na misokoto 826 ya bangi yenye uzito wa kilogramu 2.8
0 comments:
Post a Comment