Wasimamizi wa Kamati ya Olimpiki nchini Kenya, NOCK, wameshtakiwa kwa njama za wizi na usimamizi mbaya wa fedha na sare za kikosi cha Kenya katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Rio , Brazil mwaka uliopita.
Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka nchini Kenya, ODPP imetangaza kuwa, baada ya kutathmini uchunguzi, maafisa hao wanastahili kushtakiwa kwa makosa hayo.
Wasimamizi hao wakiwemo msimamizi wa timu ya Kenya kwenye Olimpiki, Stephen Soi, aliyekuwa naibu mkuu wa ujumbe wa Olimpiki, Bernard Ekumbo, katibu mkuu, FK Paul na naibu meneja wa timu hiyo, Pius Ochieng watafikishwa mahakamani baadaye mwezi huu kujua hatma yao.
Mwaka uliopita, maafisa wa polisi walinasa sare za wanariadha katika makazi ya naibu mwenyekiti, Ben Ekumbo kufuatia malalamiko ya wanariadha kuwa hawakupokea sare za kutosha.
Aidha, baadhi ya maafisa wengine wa kikosi cha Kenya kwenye Olimpiki, walieleza kudhalilishwa katika mashindano hayo kwa kutopewa makazi mjini Rio na kuishi katika hali duni.
Kikosi cha Kenya kilikumbwa na sakata mbalimbali licha ya kuandikisha matokeo mazuri kwenye mashindano ya Olimpiki.
Licha ya changamoto hizo, wanariadha wa Kenya walifanya vyema na kuondoka na medali 6 za dhahabu, 6 za fedha na moja ya shaba na kuandikisha matokeo bora zaidi ya Kenya kwenye Olimpiki.
Kesi dhidi ya wanne hao itasikizwa tarehe 31 mwezi huu kabla ya kuendelea tena tarehe 26 mwezi ujao wa Juni.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment