Image
Image

Watu zaidi ya 100 wauawa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Zaidi ya watu 100 wameuawa katika kipindi cha juma moja lililopita kusini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Umoja wa Mataifa umesema mapigano kati ya makundi ya waasi yanayochochewa na uhasama wa kidini yanasambaa. 
Mapigano yalizidi kupamba moto siku ya Jumatatu katika mji wa Bria ulioko kilomita 300 kutoka kwa mji wa mpakani wa Bangassou na kuwalazimu kiasi ya raia 1,000 kutafuta hifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa.
Hospitali ya shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres MSF iliyoko Bria kufikia jana ilikuwa imepokea watu 24 waliojeruhiwa huku mapigano yakiendelea. Mkuu wa MSF katika Jamhuri ya Afrika ya Kati Frederic Lai Manantsoa amesema imekuwa vigumu kuthibitisha idadi kamili ya waathiriwa kutokana na ghasia zinazoendelea na kuwa eneo hilo ni vigumu kulifikia.
MINUCSA yadhibiti hali
Kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA kimesema kimeidhibiti hali katika mjii wa Bangassou baada ya shambulizi la wiki iliyopita ambapo takriban watu 30 wakiwemo wanajeshi 6 wa MINUSCA waliuawa na kusababisha maelfu ya watu kuyatoroka makazi yao.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema ripoti walizozipokea ni kuwa zaidi ya watu 100 wameuawa kusini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya makundi ya waasi ya Anti Balaka na Seleka kupigana.
Hadi watu 8,500 wameachwa bila ya makazi kufuatia mapigano hayo makali. Maelfu ya watu wanaotoroka mapigano hayo yanayoendelea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanamiminika katika nchi jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wakitokea mji wa mpakani wa Bangassou.
Maelfu watorokea Congo
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR limesema mmiminiko huo wakimbizi ni mkubwa na takriban watu 2,750 waliwasili kaskazini mwa Congo mwishoni mwa wiki iliyopita na wengine wengi bado wanawasili.
UNHCR imesema Congo ambayo yenyewe inakumbwa na ghasia tangu mwishoni mwa mwezi Machi, inawahifadhi wakimbizi zaidi ya laki moja kutoka Jamhuri ya Afrika ya kati, wengi wao wakiwasili wakiwa na majeraha na bila ya mali zao.
Umoja wa Mataifa ulituma wanajeshi 10,000 na polisi 2,000 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, mojawapo ya mataifa masikini barani Afrika baada ya nchi hiyo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 kufuatia kung'olewa madarakani kwa Rais Francois Bozize.
Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Zeid Ra'ad al Hussein ameonya kuwa ghasia ambazo zinayakumba maeneo ya vijijini ambayo yalinusurika umwagaji wa damu ulioshuhudiwa vita hivyo vya Jamhuri ya Afrika ya kati vilipoanza, ni jambo la kutia wasiwasi mkubwa na kuongeza kama kawaida ni raia wa kawaida wasiokuwa na hatia ndiyo wanaathirika pakubwa.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment