Mcameroon huyo aliyesaini miaka miwili kuitumikia Simba, mkataba wake unaisha Julai mwakani, ambapo kuna kila dalili ya kutoongeza mkataba huo kutokana na anavyosemwa na kusimangwa na mashabiki kila kukicha mitandaoni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Omog alisema amechoka kusikia kila siku jambo jipya kuhusu yeye, mara anatimuliwa mara hafai.
“Naamini Simba ina viongozi waelewa na wakiamua kuachana nami watafuata utaratibu, nipo tayari kwa lolote watakaloamua.
“Natambua sisi makocha tunaajiriwa na kufukuzwa, hivyo nimejiandaa na lolote linalokuja mbeleni,” alisema.Kocha huyo amekua katika kipindi kigumu tangu kuanza kwa ligi kuu msimu huu, akisakamwa na mashabiki kwamba uwezo wa kuifundisha Simba umeshuka.
Mpaka sasa akiendelea kusakamwa, Simba ipo kileleni ikiongoza ligi kwa pointi 16 sawa na watani wao Yanga, wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, wote hawajapoteza mechi hata moja kama Azam na Mtibwa, wametoka sare michezo minne na kushinda michezo minne, hali inayoleta msuguano kileleni.
Omog pia alishangazwa na taarifa zinazosambaa kuwa ameomba ruhusa aende kwao kupumzika, alisema hizi ni taarifa potofu na watu hao hawana nia njema naye.
“Mimi naendelea na majukumu yangu kama yanavyojiainisha katika mkataba wangu na haya yanayoendelea hayaninyimi usingizi, makocha tuna changamoto kubwa na hizi ni mojawapo.
“Kama itafika muda nitaondoka, pia suala la kuongeza mkataba mwingine kwa sasa sitaweza kuzungumza sina haraka nalo, tujikite na kuangalia yapi yanayoikabili Simba katika michezo yake,” alisema.Alieleza kuwa haangalii suala jingine zaidi ya kuendelea kukinoa kikosi cha timu yake, kufikia malengo ya kuhakikisha msimu huu Simba inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alibainisha kuwa hataondoka Simba mpaka watakapoamua kumfukuza, kwani anaelewa nini anafanya na hatakatishwa tamaa.
Kocha huyo aliyejiunga Simba Julai mwaka jana, ameisaidia timu hiyo kurudi kushiriki michuano ya kimataifa, baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho.
0 comments:
Post a Comment