Image
Image

TPA yasema ushirikiano wa kibiashara kati yake na Zambia umeimarika.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imesema ushirikiano wa kibiashara kati yake na Zambia umeimarika, ambako mizigo yake inayopita katika bandari hiyo imeongezeka kutoka tani 1,248,000 kwa kipindi cha Januari hadi Septemba, 2016 hadi tani 1,478,000 kwa kipindi kama hicho mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Lydia Mallya aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ujumbe wa wafanyabiashara 10 kutoka Zambia ambao wanapitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam. “Mizigo hii inapita kwenda nchi za nje na pia wanaingiza kutoka nchi za nje ikiwemo shaba, mafuta, mahindi, mbolea na ngano na dhumuni la wao kuja hapa ni kuona jinsi bandari ilivyozidi kuboreshwa na usalama uliopo,” alisema Mallya.

Alisema bandari hiyo ina usalama wa hali ya juu na kuwahakikishia wafanyabiashara hao kutoka Zambia kwamba TPA itaendelea kuhudumia mizigo yao kwa asilimia 100 na watakuwa wanafanya nao kazi kwa karibu ili kuzidi kuvutia shehena nyingi zaidi inayotoka Zambia. “Bei zetu za huduma ni shindani ukilinganisha na bei za bandari nyingine kwa hiyo hatuna hofu, tunawakaribisha kwa mahojiano zaidi na tumewaambia mtu akiwa na mzigo mkubwa zaidi atapata bei ambayo ni nzuri ili wazidi kupitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam,” alifafanua.

Aliongeza, “Kwa kweli mzigo wa Zambia ni mkubwa sana unaopita katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa sababu kuna shehena kubwa ya shaba inapita katika bandari yetu, pia tunapokea mbolea nyingi ambayo inaenda Zambia... ukiangalia umbali wa hapa na China ni karibu zaidi kuliko bandari nyingine.”

Alisema baada ya kuzungumza na kujadiliana nao kwa kina, waliwatembeza na kuwaonesha huduma zinazotolewa na Bandari ya Dar es Salaam ikiwamo kuangalia mizigo inavyohudumiwa katika Kitengo cha Makasha, magari, mbolea, mafuta na eneo linalowekwa mizigo kwenye makontena ili kuisafirisha kupeleka nje ya nchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA, Lazaro Jacoba alisema masuala ya usalama kwa bandari zinazosimamiwa na TPA yameimarishwa ambapo serikali yenyewe imetoa msukumo mkubwa na hivyo kuwekwa mifumo sahihi ya kuhakikisha usalama wa mizigo ya wateja usio wa wasiwasi.

“Mfano Bandari ya Dar es Salaam ina mfumo wa kiusalama wa kisasa na sina hakika kama kuna taasisi nyingine nchini ina mfumo huu ambao ni unganishi wa kitehama ambao unafanya kazi ya ulinzi na kazi ya utekelezaji wa mizigo uende pamoja,” alisema Jacoba.

Alisema mfumo huo unaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa na kamera za usalama (CCTV) zaidi ya 400 na mifumo mingine ya ugunduzi wa kielektroniki unaofanywa taarifa za matukio zisambae kupitia simu za mikononi na mifumo mingine ya mawasiliano.

“Changamoto ya wizi inaonekana siyo ya bandari ila ni mizigo ya barabarani lakini kwa kuwa wateja wamesema baada ya kugundua bandari ni salama, lakini wateja wanapata changamoto barabarani tuliteua wataalamu wa usalama wa vyombo vyote vya ulinzi Tanzania ambao kwa maelekezo ya serikali wapo bandarini,” alieleza.

Alisema wataalamu hao walizunguka kutazama njia zote mpaka kwenye mipaka ya Tanzania na wateja wao na waligundua mambo kadhaa yanayosababisha upotevu wa mizigo barabarani, ikiwemo kutumwa wawakilishi na madereva wasio waaminifu.

“Tumechukua hatua na kwa sasa hali ya barabara hizo ni salama na mawasiliano ni mazuri na makamanda wa mikoa yote tunashirikiana nao na pia tunaifuatilia mizigo ikiwa barabarani kwa kutumia mifumo yetu, hivyo hali ni nzuri na kazi ya kupambana na uhalifu ni endelevu,” aliongeza.

Naye Kaimu Meneja wa Bandari, Ahmad Mchalaganya alisema kuhusu wizi wa mizigo wamejiimarisha kiulinzi na mizigo inayoenda nje wamefunga vifaa kwa ajili ya kuangalia mizigo njiani ili kudhibiti wizi.

Mapema, Kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Rais wa Chama cha Biashara na Viwanda Zambia, Michael Nyirenda alisema wataendelea kushirikiana na mamlaka hiyo kibiashara, huku akiomba wasafirishaji wa Zambia waruhusiwe kuingia Tanzania na kufanya biashara.

Aidha, Makamu wa Rais Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio aliipongeza TPA kwa kuimarisha usalama bandarini na kufunga kamera na kuboresha mifumo yao pamoja na kupunguza muda ambao mzigo unatolewa ndani ya bandari.

Alisema hali hiyo imewavutia zaidi wafanyabiashara wanaoitumia bandari hiyo wakiwemo kuutoka Zambia kuendelea kufanya kazi na TPA. “Ni majukumu yetu bandari na wadau kukaa chini na kuangali ni kitu gani walikuwa wanafaidika katika hizo bandari zingine ili na sisi tuwapatie huduma bora zaidi ili kuhakikisha mizigo yote inayoingia na kutoka Zambia inapita katika Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Urio.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment