Image
Image

"Uamuzi wa Nyalandu kubwaga manyanga CCM wawachanganya"

SIKU mbili baada ya kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiuzulu ubunge kwa aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, umeibuka mkanganyiko kuhusu uamuzi wake huo.
Kuibuka kwa mkanganyiko huo, kumekuja baada ya Ofisi ya Bunge kutoa taarifa kwa umma, kwamba Spika wa Bunge, amepokea barua ya kuvuliwa kwa uanachama wa CCM kwa Nyalandu na si ile ya kujiuzulu kwa ubunge kama alivyothibitisha mwanasiasa huyo juzi.
Taarifa ya Bunge iliyotolewa jana, ilieleza kwamba Bunge lilipokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM ikieleza kwamba tangu Oktoba 30, mwaka huu, kilimvua uanachama Nyalandu, huku mwanasiasa huyo akieleza kuwa barua ya kujiuzulu kwake ameshaiwasilisha kwa Spika.
Hata hivyo, baada ya uamuzi huo wa Nyalandu juzi, Spika wa Bunge, Job Ndugai alinukuliwa na kituo kimoja cha redio akisema kuwa bado hajapokea barua ya mwanasiasa huyo kujiuzulu ubunge, huku akimtaka aache kuwashwawashwa.
Spika Ndugai, alisema bado anaendelea kumtambua Nyalandu kama mbunge halali na mwenye stahiki zote kwa mujibu wa utaratibu.
KAULI YA POLEPOLE
Saa chache baada ya uamuzi huo wa Nyalandu, Katibu wa Itikadi na Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliibuka na kutoa video yake akielezea kwamba kuondoka kwa Nyalandu kumewapunguzia kazi za kumjadili kwenye vikao.
Polepole alisema kuondoka kwa Nyalandu hakuna jambo kubwa ambalo limetokea, bali ni la kawaida sana na kwamba waliondoka watu wazito na chama kimebaki kama kilivyo, hivyo mwanasiasa huyo si kati ya wazito bali ni mwananchi wa kawaida.
“Wapo ambao katika kipindi hiki watashindwa mwendokasi katika kusimamia ajenda za wananchi kifikra na kimatendo, hawa wanatupunguzia kazi ya kuwajadili kwenye vikao vya chama kwa kushindwa kuenenda na mwendokasi tunaoenenda nao katika nafasi zao walizopewa dhamana,” alisema Polepole.

TAARIFA YA BUNGE
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Bunge jana, ilisema Spika amepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM ya Oktoba 30, mwaka huu, ikimwarifu kwamba Nyalandu amepoteza sifa za uanachama, hivyo amepoteza nafasi zote za uongozi wa ndani wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya chama hicho.
Ilisema kwa muda sasa chama hicho kilishaanza kumchukulia hatua za kiudhibiti na kinidhamu dhidi ya vitendo na kauli zake zisizoridhisha kinyume cha misingi, falsafa na itikadi ya CCM.
Mbali na hilo, taarifa hiyo pia ilisema kuwa Ofisi ya Spika haijapokea barua kutoka kwa Nyalandu ambayo amekuwa akieleza kuwa amemwandikia Spika kumtaarifu kujiuzulu kwake tangu Jumatatu wiki hii.
“Hivyo, CCM kuanzia tarehe ya barua yao kimemjulisha Spika kuwa Lazaro Nyalandu amepoteza sifa za uanachama wa CCM, hivyo kupoteza nafasi zote za uongozi wa ndani wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya chama hicho.
“Spika, angependa kuwaarifu Watanzania kwamba kwa barua hiyo toka mamlaka halali ndani ya CCM, ambacho Lazaro Nyalandu alipata ubunge kwa mujibu wa Ibara ya 71 (1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ibara hiyo inatamka kwamba; mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake cha ubunge iwapo litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo: (f) Iwapo mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa Mbunge,” ilisema barua hiyo.
Kutokana na hilo, barua hiyo ilisema kuwa Nyalandu si mbunge tena na hatua stahiki za kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zinaendelea kuchukuliwa.
Hata hivyo barua hiyo haikuweka wazi lini tume hiyo itaarifiwa rasmi kuhusu suala hilo.
MAJIBU YA CCM
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ili atoe ufafanuzi wa suala hilo, simu yake ya mkononi haikupatikana.
Alipopigiwa simu Naibu Katibu Mkuu, Rodrick Mpogolo, alisema yeye si msemaji wa chama, hivyo atafutwe Kinana au Polepole.
Polepole alipotafutwa, alisema apigiwe simu baada ya saa moja.
Hata hivyo, baada ya muda huo alitafutwa tena, lakini simu yake iliita bila kupokewa.
KATIBA YA CCM
Hata hivyo, wakati CCM ikiandika barua ya kumvua uanachama Nyalandu, chama hicho hivi karibuni kilifanya vikao vyake vya ngazi ya juu, lakini haikuwahi kutolewa taarifa ya kuhojiwa au hata kuonywa kwa mwanasiasa huyo, jambo ambalo bado limeendelea kuzua maswali kwa umma.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 2005, Ibara ya 14 (4) haki za mwachama ambaye ana makosa kwa mujibu wa utaratibu zimeelezwa wazi.
Kwamba mwanachama ana haki ya kujitetea au kutoa maelezo yake mbele ya Kikao cha CCM kinachohusika katika mashtaka yoyote yaliyotolewa juu yake, pamoja na haki ya kukata rufani ya kwenda katika kikao cha juu zaidi cha CCM kama kipo endapo hakuridhika na hukumu iliyotolewa.
Kutokana na hali hiyo ilionekana kuwa bado kuna tatizo katika uamuzi huo wa Spika, ambao umetangazwa kwa umma, huku ufafanuzi wa kina ukiwa bado umekosekana.
MAELEZO YA NYALANDU
Jumatatu ya wiki hii, Nyalandu ambaye amekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini tangu mwaka 2000, akiwa mkoani Arusha, alitangaza kujivua nyadhifa zote za CCM na ubunge.
“Nimechukua uamuzi huu kutokana na kutoridhishwa kwangu na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya Watanzania wenzetu.
“Pia kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama), kunakofanya utendaji kazi wa kibunge wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru ulioainishwa na kuwekwa bayana kikatiba,” alisema.
Nyalandu, ambaye amepata kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kabla ya kushika wadhifa wa uwaziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema anaamini kwamba bila Tanzania kupata katiba mpya sasa, hakuna namna yoyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwapo kwa ukomo wa wazi.
“Naamini kwamba bila Tanzania kupata katiba mpya sasa, hakuna namna yoyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na mahakama ambayo ndiyo chimbuko la uongozi bora wa nchi, na kuonyesha kwa uwazi kuwa madaraka yote yanatokana na wananchi wenyewe, na kwamba Serikali ni ya watu kwa ajili ya watu.
“Mimi naondoka na kukiacha CCM, nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya uenyekiti wa UVCCM mkoa, ujumbe wa kamati za siasa wilaya na mkoa, ujumbe wa kamati ya wabunge wote wa CCM na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.“Nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo awali.
“Naamini kuwa kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna moja au nyingine, CCM nayo imekuwa chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.“Hivyo basi, kwa dhamira yangu na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya kikatiba, natangaza kukihama CCM leo hii na nitaomba ikiwapendeza wanachama wa Chadema, basi waniruhusu kuingia mlangoni mwao, niwe mwanachama, ili kuungana na Chadema na Watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kupitia mfumo wa kidemokrasia na uhuru wa mawazo.
“Vilevile, nimemua kujiuzulu kiti cha ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto lukuki nchini Tanzania.“Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo, ili kwamba sote kama taifa tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi yetu.
“Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa haki itamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo yote ya kiitikadi za kisiasa na makabila yote nchini uimarike.“Tushindane kisera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama ndugu na taifa lililo imara na nchi yenye maadili,” alisema Nyalandu.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment