Image
Image

Uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26 kugharimu Bilioni 2.5.

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu, katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Aidha, tume hiyo imeteua wagombea 177 wa vyama mbalimbali waliochukua fomu ya uteuzi namba 8C na fomu ya Maadili ya Uchaguzi namba 10, kati yao 174 sawa na asilimia 92.7 ni wanaume na 13 sawa na asilimia 7.3 niwanawake.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima alisema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika kata husika. Alitoa mfano kwamba kata yenye vituo 41, ina bajeti kubwa kuliko kata yenye vituo vikubwa. Kailima alisema katika kituo cha kupigia kura kina watendaji wanne ambao ni Msimamizi na Msimamizi Msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa kituo.
“Lakini pia kuna watu wa ziada kama Wasimamizi Wasaidizi wako ngazi ya kata na jimbo ambao wanahusika kusimamia zoezi la Uchaguzi katika maeneo husika,” alifafanua. 
Alifafanua kuwa gharama nyingine za uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka tume kwenda kwenye halmashauri husika na kutoka halmashauri kwenda kwenye kata ambako uchaguzi unafanyika.
Gharama hizo pia zinahusu utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kupitia machapisho mbalimbali ya Elimu ya Mpiga Kura na maelekezo mbalimbali kwa watendaji wa uchaguzi. “Kwenye uchaguzi huu mdogo bajeti yetu ni Sh bilioni 2.5. Siyo kwamba kila kata itatumia gharama sawa za fedha hizi, bali kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huu itatumia Sh milioni 150,” alisema Kailima.
Tume pia imeviasa vyama vya siasa vinavyohusika kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kutekeleza Sheria ya Maadili ya Uchaguzi ya 2015 waliyokubaliana kuyafuata na ameonya kuwa chama au mgombea atakayekiuka maadili hayo atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa kwenye maadili hayo ya uchaguzi. Alisema vyama vya siasa vinatakiwa kuhakikisha vinawaelimisha wafuasi, wapenzi na wanachama wao juu ya kutekeleza maadili hayo katika kipindi chote cha kampeni.
Alisisitiza kuwa iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watakiuka maadili hayo, chama husika pamoja na mgombea wake watachukuliwa hatua za kinidhamu. Alitaja baadhi ya vitendo vya kuvunja maadili ya uchaguzi ni kuchana mabango ya wagombea, kutoa lugha chafu wakati wa mikutano ya kampeni pamoja na kupitisha muda wa kufanya mikutano ya kampeni.
Alisisitiza kamati za maadili za kata na jimbo kuchukua hatua kali kwa chama au mgombea ambaye atakikuka maadili hayo. Alisema kamati hizo zinatakiwa kuchukua hatua ndani ya saa 48 mara chama au mgombea anapovunja maadili. Alizitaja baadhi ya adhabu zitazowakabili wagombea au chama ambacho kitavunja maadili ya uchaguzi kuwa ni kuomba radhi wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari kwa muda fulani wakati wa kampeni, onyo la maandishi, kusimamishwa kufanya kampeni, mgombea kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kukikuka maadili ya uchaguzi au kutozwa faini Sh 100,000.
Kailima pia alisema chama cha siasa ambacho kinataka kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni, lazima kimfahamishe msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi hilo lazima lijadiliwe na vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi. Kuhusu vitambulisho mbadala vitakavyotumika wakati kupigia kura kwa wale ambao wamepoteza kadi ya mpiga kura ambavyo ni vitambulisho vya taifa, leseni ya udereva na hati ya kusafirisha; Kailima alisema vitambulisho hivyo vitatumika tu kwa watu ambao wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika kituo husika mwaka 2015, lakini pia bado wana sifa za kupiga kura.
Akizungumzia uteuzi uliofanywa na tume hiyo wa wagombea, Kailima alisema jumla ya wanachama 155 sawa na asilimia 87.6 ya waliochukua fomu za uteuzi, walizirejesha na kuteuliwa kuwa wagombea ambapo 145 sawa na asilimia 93.6 ni wanaume na wagombea 10 sawa na asilimia 6.4 ni wanawake.
Alisema hadi mwisho wa uteuzi ulipofika saa 10.00 jioni jumla ya wanachama 22 sawa na asilimia 12.4 ya waliochukua fomu hawakuteuliwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutorudisha fomu, kurudisha fomu nje ya muda uliotakiwa kisheria na fomu kutojazwa ipasavyo.
Vyama 13 vimesimamisha wagombea ambapo CCM imesimamisha wagombea 43 sawa na asilimia 100, ikifuatiwa na Chadema iliyosimamisha wagombea 43 sawa na asilimia 98, ACT-Wazalendo wagombea 18 sawa na asilimia 40 na CUF wagombea 30 sawa na asilimia 70. Vyama vingine ni ADATADEA mgombea mmoja (asilimia 2), ADC wanne (asilimia 7), CHAUMA mmoja (asilimia 2), DP watatu (asilimia 5), NCCRMAGEUZI sita (asilimia16), NRA wawili (asilimia 5), SAU wawili (asilimia 5), TLP mmoja (asilimia 2) na UDP wawili (asilimia 5).
Aidha, alifafanua kuwa jumla ya wagombea 30 sawa na asilimia 19.4 ya wagombea walioteuliwa waliwekewa pingamizi na wagombea wenzao na Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na sababu mbalimbali. Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi, kampeni za uchaguzi tayari zimeanza na zitaendelea hadi Novemba 25, mwaka huu ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya uchaguzi.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment