Mwezi uliopita, Kigwangalla alifanya ziara ya kushitukiza bandarini hapo baada ya kupata taarifa kuwa kuna shehena hiyo ya magogo ambayo umiliki wake ulikuwa na utata. Alieleza magogo hayo 938 yamekuwa bandarini hapo kwa miaka 10 na mengine kwenye makontena 55 yapo hapo kwa miaka miwili.
Kutokana na utata huo, Kigwangalla alitoa siku 30 kwa wamiliki wa makontena 55 kujitokeza wakiwa na nyaraka zote ili kuthibitisha kama kweli yalivunwa Zambia kama ilivyodaiwa.
Alisema kushindwa kujitokeza na kuthibitisha hilo ndani ya muda waliopewa, magogo yote yangetaifishwa na kuwa mali ya serikali. Alipoulizwa kuhusu hatma ya magogo hayo baada ya siku 30 alizotoa kwisha, Waziri Kigwangalla alisema kuwa hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kuthibitisha umiliki wake.
“Kulikuwa na vikao mbalimbali ndani ya serikali kujadili suala hilo, na tumekubaliana kuyauza baada ya wahusika kutojitokeza kuthibitisha umiliki wake,” alieleza Waziri. Alisema jukumu la kuyauza magogo hayo wamepewa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wanaoruhusiwa kisheria kufanya kazi hiyo.
TRA watashirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS). Alisema siku rasmi ya kuuzwa kwa magogo hayo itajulikana hapo baadaye baada ya taratibu zake kukamilika. Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo alisema magogo ambayo yako kwenye mpango wa kuuzwa ni 938.
Yaliyomo kwenye makontena 55 hayatauzwa kwa sasa kwa kuwa kuna kesi ya msingi na uchunguzi unaendelea. Prof Silayo alisema thamani halisi ya magogo 938 haijulikani, kwa kuwa wamiliki wake ambao wana nyaraka za mzigo huo hawakujitokeza.
Alisema kutokana na hali hiyo, thamani ya magogo hayo itajulikana baada ya tangazo la kuuzwa kutoka. Alisema tangazo litakapotoka watapata fursa (TFS) ya kupima gogo moja moja ili kujua ukubwa wake, aina ya mti na ndipo thamani ya magogo yote itakapojulikana.
Awali, Waziri alisema taarifa za kiintelejensia alizopata, zinadai magogo hayo mara nyingi huvunwa Rukwa na kisha kupitishiwa nchini Zambia halafu huingizwa tena hapa nchini. Alisema watu hao wakiwa Zambia husema magogo hayo wameyavuna Tanzania na wakiwa Tanzania husema wameyavuna nchini Zambia.
Kutokana na sintofahamu hiyo, aliagiza wamiliki wajitokeze na nyaraka zinazoonesha kweli magogo hayo yalivunwa nchini Zambia na uhalali wa umiliki wao, lakini hawakutokea. Kuhusu matumizi ya magogo hayo, Waziri alisema hutumika kutengeneza vitu mbalimbali kama vile samani, dawa pamoja na marashi.
0 comments:
Post a Comment