AZAM FC imewasili salama nchinio Morocco tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji, FAR Rabat, Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi wiki hii.
Azam, imewasili Cassablanca, majira ya saa 9:15 za huku Alasiri, sawa na saa 10:15 za Afrika Mashariki na kusafiri kwa basi kwa saa mbili kwenda Rabat, mji ambao mechi itachezwa.
Azam imetua Morocco ikitokea Dubai, UAE ambako ilifika usiku jana saa 6:00 kwa saa za huko sawa na saa 5:00 kwa saa za Afrika Mashariki, ikitokea Dar es Salaam.
Ni safari ndefu iliyohusisha mabara mawili, kutoka Afrika, Tanzania kupitia Asia Dubai na kurudi Afrika nchini Morocco.
Azam imefikia katika hoteli ya Golden Tulip, maeneo ya Rabat, kaskazini mwa Cassablanca, kilomita 120 kutoka Uwanja wa Ndege wa Cassablanca, umbali wa takriban saaa mbili.
Azam itaanza rasmi mazoezi kesho kujiandaa na mchezo huo, ambao wanatakiwa kutoa sare ya mabao au kushinda ili kusonga mbele, baada ya awali katika mchezo wa kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Japokuwa hilo linachukuliwa kama jambo gumu mbele ya wengi, lakini rekodi ya timu hiyo, mali ya bilionea Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inaonyesha linawezekana.
Azam imekuwa ikicheza vizuri na kupata matokeo mazuri katika mechi za ugenini kwenye michuano hii, kuliko nyumbani na hata kufuzu kwake hadi hatua hii zaidi kulitokana na matokeo ya mechi za ugenini.
0 comments:
Post a Comment