Waziri
wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji, ameshangazwa na wimbi la uuzaji wa dawa za
nguvu za kiume uliojitokeza katika maeneo ya misikiti visiwani humu.
Akifunga mjadala kuhusu ripoti ya
Kamati ya Maendelo na Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto ya mwaka 2012/2013 ,
Duni alisema waganga wamevamia maeneo ya misikiti na kuuza dawa za kienyeji
zinazodaiwa kuongeza nguvu za kiume.
Duni alisema inashangaza kuna dawa
zinazouzwa na za wanaume pekee lakini akasema ni jukumu la wananchi wenyewe
kuwa makini kwa vile siyo kila daktari wa tiba asilia anaweza kutibu kila aina
ya maradhi.
Hata hivyo, alisema kwa upande
mwingine, vyombo vya habari vimekuwa vikichangia kuwaingiza wananchi katika
matumizi ya dawa ambazo hazijathibitishwa ubora wake kutokana na kutangaza bila
kupata ukweli wa dawa hizo.
Alisema baadhi ya dawa zinazouzwa
huchangia matatizo ya wagonjwa kutokana na kuzitumia bila maelekezo ya
kitaalam, hivyo wanapozidiwa na kwenda hospitali, ugonjwa huwa mkubwa na
wengine kupoteza maisha.
Hata hivyo, Duni alisema ataendelea
kusimamia ukweli kwa vile umri wake unafikia ukingoni.
Alisema serikali imeshatunga Sheria
ya Afya ya Jamii na Mazingira namba 11 ya mwaka 2012 ambayo itasaidia kuondoa
matatizo ya matumizi mabaya ya tiba asilia.
0 comments:
Post a Comment