Waziri wa maliasili na utalii balozi Khamis Kagasheki ametolea ufafanuzi Mgogoro wa ardhi katika eneo la hifadhi la Loliondo Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, na kusema suala la hilo linapotoshwa kwa maslahi ya baadhi ya watu.
Mgogoro huo na baadhi ya viongozi wa eneo hilo la Loliondo unafuatia uamuzi wa serikali uliotangazwa na waziri wa Maliasili na Utalii,wa kutaka kumega sehemu ya ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,500 toka eneo la kilometa za mraba 4000 zilizopo kwenye eneo la hifadhi la Loliondo Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, na kuamua kutenga kilometa za mraba 1500 za ardhi kwa ajili ya uhifadhi wa taifa.
![]() |
| Balozi Khamis Kagasheki - Waziri wa Maliasili na Utalii |
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini dar es salaam leo, Balozi Kagasheki amesema upotoshwaji huo unafanywa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wanaojipambanua kushughulikia masuala ya ardhi hatua inayojenga dhana ya kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa ardhi wakati kilichofanyika ni utekelezaji wa sheria iliyopo ambayo inajulikana kwamba kwa kuzingatia sera yake ya uhifadhi na ya kihistoria, ardhi ni rasilimali ya taifa.
Balozi Kagasheki amefafanua kuwa kimsingi hatua hiyo ya kutaka kumega ardhi imefikiwa baada ya kufanyika kwa tathmini za kina juu ya umuhimu wa kutengwa kwa eneo hilo na manufaa yake kwa taifa..
Baadhi ya wakazi wa Loliondo wakiongozwa na viongozi wao waliofanya mikutano kadhaa na waandishi wa habari na baadhi ya maofisa wa balozi za nje nchini, wamepinga uamuzi huo wa kumega ardhi yao wanayodai wameishi kwa kipindi kirefu na kusisitiza lengo la serikali ni kumnufaisha mwekezaji wa kigeni aliyepo kwenye eneo hilo, jambo ambalo hata hivyo limepingwa na waziri Kagasheki..


0 comments:
Post a Comment