Na .Mcharo Mrutu Dar es Salaam.
Wakati tume ya mabadiliko ya katiba ikiwa katika hatua ya uchambuzi wa maoni ya wananchi pamoja na kuandika rasimu ya awali ya katiba mpya, wananchi wamehimizwa kujiandaa kufanya maamuzi magumu katika masuala ya msingi kwa taifa kama ambavyo tume hiyo italazimika kufanya hivyo hususani katika masuala ambayo yametolewa maoni yanayokinzana.
Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu Joseph Warioba ametoa wito huo leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusiana na masuala mbalimbali yanayojitokeza wakati wa mchakato wa kuandikwa katiba mpya ukiendelea ambapo kimsingi amesema zoezi la uchambuzi wa maoni linaonyesha namna wananchi wengi walivyotoa maoni tofautitofauti juu ya masuala nyeti kwa taifa ikiwemo muundo wa muungano, madaraka ya rais na mengineyo.
Jaji mstaafu Joseph Warioba - Mwenyekiti tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya |
Jaji Warioba amesema maoni mbalimbali juu ya masuala hayo yanaifanya tume kufanya maamuzi magumu kwa kuzingatia mustakabali wa nchi na kuwasihi pia wananchi kujiandaa kufanya maamuzi magumu wakati rasimu hiyo itakaporejeshwa kwao kuitolea maoni bila kujali tofauti zao za kisiasa, kidini au itikadi yoyote ile.
Akizungumzia uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya uliomalizika hivi karibuni, Jaji warioba amesema ingawa mchakato umefanyika kwa mafanikio makubwa, lakini ulikumbwa na dosari kadhaa hususani masuala ya itikadi za kidini na siasa na hivyo kutoa angalizo kwa taasisi za kidini na vyama vya kisiasa kuwaacha wananchi kuwa huru kujadili rasimu ya katiba ijayo kwa kuweka mbele utaifa kuliko maslahi ya vikundi vyao.
Katika hatua nyingine tume hiyo ya katiba inatarajia kuunda mabaraza ya katiba kwa watu wenye ulemavu yatakayokuwa na jumla ya wajumbe 40 ili kuwapa fursa walemavu kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya awali ya katiba inayotarajiwa kuwa tayari mwezi mei mwaka huu.
Jaji mstaafu Joseph Warioba - Mwenyekiti tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya |
Kwa mujibu wa tume ya mabadiliko ya katiba, uchaguzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya katika kata kwa upande wa Bara na shahia kwa upande wa Zanzibar ulikamilika kwa mafanikio ya asilimia zaidi ya 95, huku tume hiyo kukamilisha zoezi hilo la kuandika katiba mpya itakayokidhi kiu ya watanzania kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.
0 comments:
Post a Comment