Mkoani Dar es salaam, wafanyakazi wamehimizwa kuitumia siku ya Mei Mosi kutafakari juu ya kuboreshewa maslahi na haki zao pamoja na uwajibikaji wenye tija kwa watumishi wa ngazi mbalimbali ili kutenda haki kwa waajiri wao na makundi mengine katika jamii.
Shime hiyo imetolewa wakati wa sherehe za Mei Mosi zilizofanyika katika uwanja wa mnazi mmoja ziktanguliwa na maandamano ya wafanyakazi wa idara, taasisi, mamlaka, makampuni na mashirika mbalimbali ya serikali na binafsi wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti zikitaka serikali kutazama upya mishahara duni na kodi kubwa kwa wafanyakazi na tofauti kubwa ya mishahara kama kikwazo cha kupandisha ari ya kazi.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Said Meck Sadiq aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo aliwataka wafanyakazi kushirikiana na serikali kukomesha vitendo vinavyorudisha nyuma jitihada za maendeleo kwa kutimiza wajibu wao kwa uadilifu kwa kutokuruhusu mwanya wa vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo kimsingi vinainyima serikali mapato ambayo yangetumika kuboresha maslahi yao.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick, akiwa meza kuu na baadhi ya viongozi wengine wakati wakisimama kupokea maandamano hayo. |
Akisoma hotuba kwa niaba ya wafanyakazi wa Dar es salaam katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa bandari - DOWUTA Bi Abidunas Athumani aliorodhesha madai na changamoto zaidi ya kumi zinazowakabili wafanyakazi wa Dar es salaam ikiwemo ushirikishwaji katika vyombo vya kutoa maamuzi pamoja na waajiri kutowasilisha makato mbalimbali ya wafanyakazi katika mifuko inayohusika.
Akitolea maamuzi baadhi ya madai ya wafanyakazi hao, Mkuu wa mkoa aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote za Dar es salaam kuhakikisha wanamaliza kero ya makato ya fedha za wafanyakazi kutopelekwa katika mifuko inayohusika kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha mwezi june.
Sherehe hizo za mei mosi mwaka huu zenye kauli mbiu inayosisitiza umuhimu wa Katiba mpya kuzingatia Usawa, Haki na Maslahi kwa tabaka la wafanyakazi, kwa mkoa wa Dar es salaam ziliingia dosari kidogo kutokana na magari yaliyokuwa yameandaliwa kutoa maonyesho ya bidhaa na huduma mbalimbali kulazimika kubaki nje kutokana na udogo wa uwanja wa mnazi mmoja uliokuwa umefurika umati wa wafanyakazi waliojitokeza kuonyesha mshikamano.
---------------------------------
0 comments:
Post a Comment