VIWANDA vinne vya kutengeneza pombe,
kusindika maziwa na machinjio mawili yamefungwa katika wilaya za Rombo, Mwanga
na Siha mkoani Kilimanjaro kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya ubora
vilivyoainishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).
Mkaguzi wa Chakula Kanda ya Kaskazini, Abdalah Mkanza alisema ufungaji huo umefanikiwa wakati idara ya ukaguzi ya kanda hiyo ilipofanya ukaguzi wa kushitukiza kwa kushirikiana na wakaguzi wengine kutoka Kanda ya Mashariki.
Alisema ukaguzi ulifanyika kwa viwanda vyote vikubwa na vidogo mkoani Kilimanjaro na machinjio yote za mjini na vijijini ambapo walibaini wananchi wapo hatarini kupata magonjwa kutokana na mazingira halisi ya uchinjajio wa wanyama na viwanda hivyo.
Mkaguzi
huyo alisema zoezi la ukaguzi litafanyika kwa mara nyingine mkoani humo kwa
lengo la kutazama iwapo maeneo waliyoyapa maelekezo yamefuata ama la, ili hatua
nyingine ziweze kuchukuliwa iwapo itabainika wamepuuza.
Aliwataka
wafanyabiashara na waagizaji wengine wa bidhaa kutoka nje ya nchi kuwasiliana
na TFDA ili kujiridhisha kama wanavyoagiza au kutumia kwa ajili ya walaji
vimethibitishwa na mamlaka hiyo.
Kwa
upande wao baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusiana na kufungwa kwa viwanda vya
pombe, Johnson Swai na Habibu Juma walipongeza juhudi hizo lakini wakataka
ukaguzi huo kufanyika kila baada ya miezi sita kwani wapo wanaofungua viwanda
na kufunga mara wanaposikia wakaguzi wanapita.
0 comments:
Post a Comment