Na. Salum Mkambala, Dar es Salaam.
Hospitali ya viungo ya CCBRT iliyopo jijini dar es
salaam, imewataka wanawake wenye dalili au viashiria vya ugonjwa wa Fistula
kwenda katika vituo vya afya na hospitali zingine zinazotibu ugonjwa huo
mikoani kuchunguzwa kwanza badala ya kwenda moja kwa moja kwenye hospitali hiyo
ili kuepusha mlundikano wa wagonjwa wasio na rufaa kutoka mikoani.
Mkurugenzi wa huduma za jamii wa hospitali ya
CCBRT, bi. Brenda Msangi ametoa wito huo
jijini dar es salaam katika mahojiano maalumu juu ya mwamko wa wagonjwa wa kujitokeza kupata huduma ya ugonjwa huo
unaotajwa kusababisha ongezeko kubwa la wagonjwa wa fistula kwenye hospitali
hiyo.
Brenda Msangi - Mkurugenzi wa huduma za jamii wa hospitali ya CCBRT |
Amesema kimsingi idadi ya wagonjwa wanaojitokeza
kupata tiba imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na kampeni maalum ya mwezi
mmoja iliyofadhiliwa na kampuni ya simu za mkononi ya VODACOM na VODAFONE
Foundation ijulikanayo kama Trasport my Patient ambayo wagonjwa hugharamiwa
nauli na gharama za matibabu.
Hata hivyo amesisitiza kuwa licha ya CCBRT kutoa
huduma hizo, bado huduma pia zimesogezwa na zinatolewa kwenye hospitali za
mikoa na hata wilaya hivyo ili kupunguza usumbufu kwa wagonjwa kufuata huduma
hizo mbali.
Takwimu zilizopatikana hospitalini hapo zinaonyesha
kuwa zaidi ya wanawake 50 walifanyiwa upasuaji wa kutibu fistula kwenye
hospitali hiyo ya CCBRT katika mwezi Mei mwaka huu pekee ikiwa ni ongezeko la
zaidi ya asilimia 50 ya wanawake waliotibiwa kati ya Januari na Aprili mwaka
huu ambapo malengo ni kuwatibu wanawake 650 kwa mwaka huu kutoka wanawake 501
waliofanyiwa upasuaji mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment