Serikali imewahimiza wazazi, vijana na wananchi kwa
ujumla kuhakikisha wanatokomeza biashara ya dawa za kulevya ndani ya jamii, kwa
kuwa biashara hiyo haramu inaathari kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii pia.
Rai hiyo imetolewa mjini Dodoma na Waziri Mkuu bw.
Mizengo Pinda katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, Bw. William Lukuvi, katika
maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya duniani.
Aidha, Waziri Mkuu amewaonya wale wote walio na mpango
wa kuingia katika biashara hiyo, kutambua kuwa serikali ipo macho, na
itawachukulia hatua za kisheria, huku wale watakaopatikana na hatia, watapata
kifungo cha maisha.
Kwa upande wake,
Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Daw za Kulevya, Bw. Christopher
Shekiondo, amesema kwa sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kilimo
cha bangi, ambacho ndicho kinachochochea matumizi ya dawa za kulevya kwa
vijana.
Naye, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi
akapendekeza kutafutwa takwimu za wale wanaofanya biashara hiyo haramu, kama
kweli watoto wao wanatumia dawa hizo, kwa kuwa madhara makubwa wanayaleta
kwenye jamii.
Katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo
Furahia Afya Yako na Si Dawa za Kulevya, vijana wawili, Robert Mbeho kutoka
Dodoma na Nuru Salehe kutoka Zanzibar walitoa ushuhuda, jinsi dawa hizo
zilivyotaka kuwapotezea ndoto zao.
0 comments:
Post a Comment