Mkuu wa sera za kigeni wa EU, Catherine Ashton akiwa na Mohamed ElBaradei jijini Cairo.
Mkuu wa Sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya EU, Catherine Ashton
amekutana na Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani, Mohamed Morsi wakati huu
ambapo wafuasi wake wameendelea na maandamano jijini Cairo. Vyanzo vya habari
nchini humo vimesema kuwa Ashton amekutana na Morsi ambaye hajawahi kuonekana
hadharani tangu alipopinduliwa tarehe 3 mwezi Julai.
Msemaji wa Ashton Maja Kocijancic amesema kiongozi huyo amezungumza na
Morsi kwa masaa mawili mfululizo katika eneo la siri ambalo kiongozi huyo
amehifadhiwa.
Ashton aliyewasili jijini Cairo mwishoni mwa juma lililopita amekuwa
na mazungumzo na viongozi kadhaa wa Taifa hilo akiwamo Rais wa serikali ya
mpito Adly Mansour, Makamu wa Rais katika wizara ya mambo ya nje Mohamed ElBaradei
na Mkuu wa Jeshi Generali Abdel-Fattah al-Sisi.
Hofu ya usalama imeendelea kutanda nchini humo hasa mara baada ya
mauaji ya watu zaidi ya sabini mwishoni mwa juma lililopita.
Maandamano ya wanaomuunga mkono Morsi yameendelea kufanyika ambapo
waandamanaji walizunguka ofisi za usalama, ingawa kulitolewa onyo kwa
waandamanaji kutotumia vibaya haki yao ya kuandamana.
Mashirika yasiyo ya kiserikali yametoa ombi la kutaka Waziri wa mambo
ya ndani wa nchi hiyo, Mohamed Ibrahim atimuliwe kazi na kushtakiwa kutokana na
kushindwa kudhibiti mauaji hayo.
Walinda usalama nchini humo bado wanashutumiwa kutumia silaha nzito
dhidi ya waandamanaji, taarifa ambazo zimeendelea kukanushwa na wizara ya mambo
ya ndani wakidai hutumia mabomu ya kutoa machozi pekee katika kutawanya
waandamanaji.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Ban Ki Moon aliitaadharisha serikali ya mpito kuwa mauaji ya
waandamanaji nchini humo yanakwamisha juhudi za kutatua mgogoro huo unaoendelea
kutatiza nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment