Kipa chaguo la kwanza wa timu ya taifa ya soka ya
Tanzania (Taifa Stars), Juma Kaseja, ambaye hivi sasa yuko huru baada ya
kumaliza mkataba wake wa kuidakia Simba amepata ofa nono ya dola za Marekani
30,000 (Sh. milioni 50) kutoka kwa klabu ya FC Lupopo inayoshiriki Ligi Kuu ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili aanze kuitumikia msimu ujao, imefahamika.
Kaseja amepata ‘ulaji’ huo kufuatia uongozi wa Lupopo
kuachana na kipa wa Mtibwa Sugar, Hussein Shariff ‘Cassilas’ ambaye
hawakukubaliana dau la uhamisho na klabu yake ya Mtibwa ya Manungu, Turiani
mkoani Morogoro.
Inadaiwa kuwa Lupopo walikuwa tayari kumsajili Shariff
kwa dola za Marekani 20,000, lakini baadaye Mtibwa Sugar walitaka kiasi kama
hicho ili wavunje mkataba naye jambo ambalo klabu hiyo ya Kongo haikuwa tayari
kwani maelezo ya awali waliyokuwa nayo ni kwamba kipa huyo alikuwa hana timu.
Habari zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam
zinasema kuwa Kaseja ambaye alimaliza mkataba wa kuichezea Simba tangu Juni 30
mwaka huu atalipwa mshahara wa kila mwezi wa dola za Marekani 2,000 (Sh.
milioni 3.2), kiasi ambacho inadaiwa ni kikubwa kulinganisha na mshahara
aliokuwa akilipwa na klabu yake ya zamani ya ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Chanzo hicho kilifichua zaidi kwamba uongozi wa Lupopo
tayari umeshafanya mazungumzo ya awali na Kaseja na hivyo kipa huyo nyota wa
Stars anasubiriwa afike ili amalizane nao na kusaini mkataba.
“Hata hivyo, watu wa Lupopo wamekuwa wakimbembeleza
kipa huyo ili wampe mkataba wa miaka miwili… mwenyewe Kaseja anataka asaini
mkataba wa kuichezea kwa mwaka mmoja tu, ila dalili zinaonyesha watakubaliana
kwavile hii ni ofa nzuri kwake (Kaseja) kwa wakati huu,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na NIPASHE kutokea Kampala jana mchana,
Kaseja alikiri kufanya mazungumzo na timu moja ya nje ya nchi na nyingine
kadhaa za hapa nchini, lakini hakutaka kuzitaja timu hizo kwa maelezo kuwa bado
hajahitimisha majadiliano.
Kaseja alisema vilevile kuwa baadhi ya timu
zimeshindwa kufanya naye mazungumzo rasmi kwa kuhofia gharama za kumsajili,
ingawa wengi wao wameonyesha kuwa kiufundi wanamhitaji sana.
“Hapa bongo zipo timu zinanisubiri nirudi ili tufanye
mazungumzo na klabu moja ya nje ya nchi pia inanihitaji. Sema timu nyingi
zinaniogopa kwavile wanahisi kwamba siwezi kuzikubalia au labda nitataka pesa
nyingi kutokana na uzoefu wangu langoni,” alisema Kaseja.
Ingawa Kaseja hakutaja timu zinazomhitaji, lakini
inafahamika wazi kuwa mojawapo ni klabu ya Mbeya City ya Mbeya iliyopanda
daraja na kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.
Kocha wa klabu hiyo,
Juma Mwambusi, amekuwa akisema kuwa wanamuhitaji kipa huyo kwavile bado yuko
katika kiwango cha juu na uzoefu wake utawasaidia sana kikosini.
Licha ya kuidakia Simba kwa takriban muongo mmoja,
Kaseja pia aliwahi kuzichezea Moro United iliyokuwa Morogoro na Yanga
aliyoitumikia kwa msimu mmoja.
0 comments:
Post a Comment