Hassan Abbas. |
Tanzania imepongezwa na Umoja wa Afrika (AU) kwa hatua
kadhaa ilizofikia katika kuimarisha utawala bora, ikiwa ni utekelezaji wa
Mkataba wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Ofisa Habari wa APRM, Hassan Abbas, alisema pongezi hizo
zilitolewa katika wasilisho la ripoti ya nchi iliyowasilishwa na Rais Jakaya
Kikwete mbele ya viongozi wenzake wa Umoja huo Januari 26, mwaka huu jijini
Addis Ababa, Ethopia.
“Tayari Tanzania tumeshakamilisha zoezi hili la kwanza
la aina yake na uzinduzi rasmi wa ripoti hiyo utafanyika Oktoba, mwaka huu na
serikali imepewa muda wa kufanyiakazi maeneo yenye changamoto,” alisema.
Alisema tayari serikali imeonyesha dhamira ya dhati kwa kuanza utekelezaji wa maoni mbalimbali ya wananchi kama vile kuendelea kusimamia utekelezaji na kuripoti kwa umma na baada ya uzinduzi wa ripoti, masuala mengine kuingizwa katika mipango na bajeti za miaka ijayo za wizara na taasisi nyingine husika.
Baadhi ya masuala yaliyobainishwa na ambayo yanahusu
katiba yaliwasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na mengi yameingizwa
kwenye rasimu iliyotolewa hivi karibuni pamoja na mengine kuingizwa kwenye
mfumo wa mpango wa mwaka na bajeti ya serikali iliyopitishwa hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment