Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amewataka watu kuiga
mchango wa Mandela na kujitolea kwake, kwa kuongeza juhudi za kuiendeleza jamii
yao. Zuma mwenyewe atawakilisha mtazamo wa Mandela wa kuzileta pamoja jamii,
kwa kuwapa nyumba watu masikini weupe.
Katika juhudi hizo, waendesha baskeli watafanya usafi
mitaani, wafanyakazi wa kujitolea watapaka shule rangi, na wanasiasa
watashiriki katika miradi mingine ya kujitolea kwa muda wa dakika 67, kutambua
miaka 67 ambayo Mandela amekuwa mtumishi wa umma.
Aidha, wanafunzi wataanza
siku yao shuleni kwa kuimba wimbo '' Happy Birthday Mandela'' wakimtakia heri
na kumpongeza kwa kutimiza umri huo wa miaka 95.
Shughuli nyingine itakayofanyika kuadhimisha miaka 95 ya
Nelson Mandela, ni kumkabidhi mkongwe huyo kitambulisho kipya cha kisasa,
ambacho kitapokelewa kwa niaba yake na bintiye Zindzi.
Kumbukumbu ya mapambano dhidi ya ubaguzi.
Mandela anasifiwa kote duniani kwa kusimama kidete dhidi ya
ubaguzi wa aina yoyote.
Tukio hilo litakuwa na viashiria mbali mbali kama kumbu
kumbu ya enzi za ubaguzi wa rangi, ambapo raia weusi walilazimishwa kubeba
vitambulisho, na hawakuruhusiwa kutembea katika baadhi ya maeneo, kwa baadhi ya
nyakati.
Mwaka 2010, Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe 18 Julai
kuwa siku ya Mandela, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel ya Amani, lakini
mwaka huu, siku hii imekuwa na umuhimu mkubwa zaidi.
Mandela amalazwa hospitalini kwa siku 41 sasa akiugua
maambukizi ya mapafu, na kwa muda mrefu hali yake imetajwa kuwa mbaya, lakini
ambayo imedhibitiwa na madaktari.
Watu wa familia yake wamesema kuwa hali hiyo imeimarika kwa
kiasi fulani, na anaweza kupumua kwa msaada wa mashine. Binti yake Zindzi jana
aliliambia shirika la habari la Sky News kwamba kuna wakati walipokuwa wamekata
tamaa wakijiweka tayari kupokea habari mbaya, na kuongeza kuwa kwa sasa anawapa
matumaini.
Watu mbali mbali mashuhuri na wa kawaida wameahidi kujiunga
na wananchi wa Afrika Kusini leo, kumuunga mkono Mzee Mandela katika siku kuu
yake ya kuzaliwa.
0 comments:
Post a Comment