Rais Kikwete ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha
zinaingiza katika bajeti zao mpango wa ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo
ili kukabiliana na ukosefu na uchakavu wa majengo ya kuendeshea kesi.
Alitoa agizo hilo
wakati wa uzinduzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Bukoba,
uliofanyika jana na kuhudhuriwa na viongozi akiwamo Jaji Mkuu, Othuman Chande
na Mawaziri.
Agizo hilo la Rais kikwete limekuja muda mfupi baada ya
hotuba ya Jaji Mkuu kueleza kuwa Mahakama za Mwanzo 960 zilizopo nchini ni 664
ndizo zinazotumia majengo yanayomilikiwa na Mahakama huku 286 zikiendesha
shughuli zake katika majengo ya taasisi nyingine za Serikali.
Hata hivyo alisema mahakama hizo baadhi zinatumia majengo ya
Serikali za vijij,kata na majengo 10 yakiwa yanakodishwa toka kwa watu binafsi.
Akizungumzia Mahakama za Wilaya, Jaji Chande alisema 27
zinatumia majengo ya taasisi mbalimbali za Serikali na mahakama tatu ziko
katika majengo ya kukodi huku Wilaya 32 nchini zikiwa hazina majengo ya
mahakama za Wilaya kabisa.
Alimweleza Rais Kikwete kuwa lengo la Mahakama kuu ni kuwa
na Mahakama Kuu katika mikoa yote chini na kwamba kwa sasa ni mikoa 13 tu ndiyo
yenye Mahakama Kuu.
Aliitaja mikoa isiyokuwa na Mahakama Kuu kuwa ni Lindi,
Shinyanga, Mara, Singida, Morogoro, Manyara, Pwani, Lindi, Geita, Simiyu,
Njombe na Katavi.
Kutokana na maelezo hayo, Rais Kikwete alisema Serikali
katika bajeti ya mwaka huu, imetenga fedha kwa ajili ya kumaliza mahakama saba
likiwamo jengo la kanda ya Bukoba ambalo lilizinduliwa jana.
Alisema Serikali imedhamiria kwamba katika kipindi cha miaka miwili, suala la ukosefu wa Mahakama Kuu liwe historia hapa nchini angalau ili kuondoa kero kwa wananchi wanasafiri mikoa mingine kutafuta haki yao.
Wakati huo huo, Rais Kikwete aliongoza Watanzania nchini
kuhudhuria maadhimisho ya mashujaa waliopigana vita vya ukombozi dhidi ya
majeshi ya uvamizi ya Nduli Idd Amini mwaka 1978/79, yaliyofanyika katika kambi
ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kaboya wilayani Muleba.
Rais Kikwete alitoa onyo kwa yeyote atakayejitia kiburi kwa
kuchokoza serikali ya Tanzania na kusema kwamba nguvu zilizomwondoa Nduli Idd
Amini ndizo hizo zitakazotumika kumsughulikia.
Aliwataka Watanzania kulala usingizi bila kuwa na hofu juu ya wachokozi.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange,
akiwasalimia wananchi waliokuwa katika viwanja hivyo, aliwatoa hofu wananchi
akieleza kwamba jeshi liko imara wakati wote na muda wote.
0 comments:
Post a Comment