VITA dhidi ya
usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia katika viwanja vya ndege
nchini iliyoanzishwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, imemvuta
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Kigwangallah, ambaye ameahidi kutaja majina
wauzaji wa dawa hizo ili kuisadia serikali kuchukua maamuzi magumu.
Dk. Kigwangala
aliliambia NIPASHE jana kwa njia ya simu kuwa hadi sasa amepokea majina saba ya
vinara wanaojihusisha na biashara hiyo na kwamba anaendelea kupokea
ushahidi ukiwamo wa picha za watu hao wanawauzia kina nani na wanakaa wapi.
Mbunge huyo
amesambaza taarifa kupitia mitandao ya jamii ikiwamo Facebook akiwataka
wananchi wenye taarifa za wauza unga kuwasiliana naye na kumpa ushahidi ili
awataje bungeni katika mkutano wa 11 wa Bunge unaoanza kesho.
Alisema zoezi la
kupokea majina hayo na ushahidi linakwenda vizuri na kwamba mwitikio umekuwa
mkubwa kutoka kwa wananchi na kusisitiza kwamba lazima awataje wahusika kwa
majina.
Aliongeza kuwa
ameandika barua kwa Spika wa Bunge kuomba fursa ya kutoa maelezo bungeni kama
mbunge na kwamba atampelekea barua nyingine ili apatiwe nafasi ya kusimama na
kutaja majina hayo.
“Mimi siogopi kitu,
nikipata ushahidi wa kina nitataja majina ya watu wote waliotajwa na wananchi
wanaoniletea ushahidi na katika hili moja ya jina ni la kinara anayetajwa tajwa
sana,” alisema Dk. Kigwangallah.
Aliwataka wananchi
wenye taarifa zinazojitosheleza kumtumia ili azifanyie kazi kabla ya kuwataja
bungeni.
Alisema shinikizo
la wanasiasa linaweza kusaidia kuiamsha serikali kupitia Jeshi la Polisi kuanza
kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.
MTAMBO MPYA
WAFUNGWA JNIA
Kufuatia malalamiko
kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Umegeuzwa uchochoro
wa kupitishia dawa hizo kwenda nje, Serikali imefunga mtambo mpya ya kisasa
utakazokuwa na uwezo wa kutambua zitakazoingizwa au kupitishwa kutoka ndani na nje
nchi.
Dk. Mwakyembe jana
alifika katika uwanja huo kukagua mtambo huo wa Rapscan 600 series na kuelezwa
na viongozi kuwa umetoka Uingereza na kufungwa kwenye uwanja huo kuanzia wiki
iliyopita.
Dk. Mwakyembe
akizungumza na NIPASHE katika uwanja huo baada ya kumaliza kukagua mtambo huo,
alisema lengo la serikali kuongeza mtambo mwingine ili kukomesha kabisa
tatizo la watu wasiokuwa waaminifu kupitishia dawa hizo katika uwanja huo na
kuliletea aibu Taifa.
Alisema Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kwa upande wake nayo imefunga mitambo yake kwa
lengo la kukabiliana na dawa hizo na kwamba kutoka na ushirikiano uliopo katika
ya vyombo vya usalama ni wazi kuwa itakuwa vigumu kwa mtu kuzipitisha JNIA.
Kwa upande wake
Meneja Usalama wa JNIA, Clemence Jingu, alimweleza Dk. Mwakyembe kuwa mtambo
huo umefungwa kitaalamu na kwamba hatua iliyobaki ni kufungwa kifaa
kijulikanacho kama Soft narc scan.
Jingu alisema
katika uwanja huo wameanzisha huduma ya kukagua mizigo ya abiria wanaoingia
nchini kutoka nchi mbalimbali nyakati za usiku ambayo awali haikuwapo .
Agosti 16, mwaka
huu Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama wanne wanaodaiwa kuhusika katika
njama za kusafirishwa dawa za kulevya na kuigiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
(TAA) kuwafuka kazi na kufunguliwa mashtaka.
Alichukua hatua
hiyo kufuatia kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8
kukamatwa Julai 5, mwaka huu nchini Afrika Kusini zikitokea Tanzania, kupitia
JNIA.
Maofisa usalama hao
ni Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana.
Pia aliliagiza
Jeshi la Polisi kumuondoa mara moja katika uwanja huo, askari wake, Ernest na
kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwenye njama za kupitisha
mabegi sita ya dawa hizo yaliyokamatwa Afrika Kusini.
Pia alisema polisi
inapaswa kumsaka Nassoro Said Mangunga aliyevikwepa vyombo vya dola Afrika
Kusini na kutoroka na mabegi matatu ya dawa hizo.
Alisema mbeba
mizigo katika uwanja huo, Zahoro Mohamed Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi,
kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ili kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka
ya jinai.
Dk. Mwakyembe pia
aliiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa
wake waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati
mwafaka kukagua mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya.
Takwimu zinaonyesha
kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara ya dawa za
kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, watuhumiwa 10,799 wamekamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.
Katika kipindi
hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika
Kusini na kuharibu taswira ya nchi na kusababisha wenzao wasio na hatia kupata
usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Wiki moja
baada ya tukio la wasichana hao kukamatwa, Watanzania wengine wawili
walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa hizo aina ya cocaine na heroine zenye
thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam
kupitia Dubai hadi Hong Kong.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment