Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema anasikitishwa na matukio ya
hujuma yaliyojitokeza Zanzibar, ikiwemo watu kumwagiwa tindikali, na kutaka
uchungunzi wa kina ufanywe kuwabaini wahusika, na baadaye ripoti ya uchunguzi
huo iwekwe wazi kwa wananchi.
Amesema hatua ya
kuwekwa bayana ripoti za uchunguzi wa matukio hayo ya hujuma, ni jambo muafaka
katika kufuta dhana zinazojengeka miongoni mwa wananchi na jamii ya kimataifa
kuhusiana na watu wanaohusika kufanya hujuma hizo.
Maalim Seif
ameyasema hayo katika mahojiano maalum juu ya maadhimisho ya miaka 50 ya
Mapinduzi ya Zanzibar tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964.
Amesema ili amani
na mshikamano wa wazanzibari udumu, matukio kama hayo ya hujuma ambayo yamekuwa
yakiwalenga zaidi baadhi ya viongozi wa dini na hata wageni, hayanabudi
kuangaliwa kwa upana wake, na kuwataka wananchi wajiepushe na kufikia maamuzi
ya haraka kuwahusisha wengine bila ya uchunguzi wa kina kufanywa.
Alisema wananchi
walipata matumaini ya kukomeshwa kwa vitendo hivyo mara baada ya hujuma
zilizofanywa dhidi ya viongozi wa dini pamoja na mripuko uliotokea katika
kanisa la Arusha ambapo walihidiwa uchunguzi wa kina utafanyika na kuhusisha
wapelelezi wa kimataifa, lakini hadi sasa hakuna ripoti yoyote iliyowekwa
bayana.
Maalim Seif
ameeleza kwamba badala yake matukio ya hujuma yameendelea na wananchi kuendelea
kujenga dhana ya kuwahusisha watu au makundi maalum bila ya kuwa na uthibisho,
jambo ambalo ni hatari kwa usalama na utulivu wan chi.
“Ingekuwa wakati
ule tungesema ni siasa, lakini sasa tuna serikali ya pamoja Zanzibar, kwa nini
mambo haya yanatokea sasa, huu ni mtihani mkubwa kwetu”, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye
pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, amesema pia amekuwa mgumu kuamini
kuwa dini inahusika katika matukio ya hujuma yaliyotokea Zanzibar.
Amesema Zanzibar
ina historia ya kipekee ya uvumilivu wa kidini duniani, kutokana na wananchi wa
visiwa hivi kuishi pamoja kwa miaka mingi bila ya kubaguana kwa misingi ya dini
zao.
“Sisi Zanzibar
kiwango chetu cha uvumilivu ni kikubwa na nambari moja duniani, hata ukiangalia
Ukristo Afrika Mashariki mlango wake ni Zanzibar”, alifafanua Maalim Seif.
Akitoa mfano wa
uvumilivu huo, Maalim Seif amesema hata unafika mwezi wa Ramadhan huwezi
kumuona mtu wa imani yoyote akila hadharani wakati wa mchana, na kwamba
wananchi wote wanashirikiana katika shughuli za kijamii bila ya kujali imani
zao.
Ameeleza kuwa baada
ya matukio ya kujeruhiwa Padri Ambrose Mkenda, kuuawa kwa Padri Evarist Mushina
mripuko wa bomu katika kanisa mjini Arusha, Serikali iliahidi kuleta makachero
wa F.B.I, na hata baada ya wasichana wa Kiingereza kumwagiwa tindikali
inaelezwa wachunguzi kutoka Scktland Yard wapo, lakini hakuna taarifa hadi sasa
iliyotolewa kuhusiana na uchunguzi huo.
“Tusiajiegemeze
kwenye dhana, uchunguzi ndio kitu muhimu. Hawa wanaoathirika na hujuma mbali ya
kuwa viongozi wa dini nao ni binadamu, tujiulize jee hawakujenga uhasama au
kutokufahamiana na wengine huko katika jamii”, alihoji Maalim Seif.
Amefahamisha kuwa
ni makosa kuendesha mambo kwa dhana, kwa vile matokeo yake ni kuwaadhibu watu
kwa kuwaweka ndani bila ya kuwa na hatia.
Amewataka wananchi
kuwa makini na waendelee kuwa wamoja, ili amani, mashirikiano na umoja uliodumu
uendelee wakati huu ambapo Zanzibar inaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.
Wakati huo huo
Maalim Seif amekutana na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen QiMan na
kuelezea umakini na uadilifu wa makampuni ya Kichina katika kutekeleza majukumu
yao.
Amesema mara nyingi
kazi za kiufundi wanazopewa wataalamu wa Kichina zimekuwa zikitekelezwa kwa
umakini na kwa wakati uliopangwa, hali inayotoa matumaini ya kuendelea kutoa
tenda kwa makampuni hayo.
Aidha amesifu
ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Zanzibar ambao umekua
ukichangia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Amemtaka balozi
huyo kuwa kiungo katika kuwashajiisha watalii na wawekezaji wa China kuja
Zanzibar, ili kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea wananchi
maendeleo.
Amesema China ni
mshirika wa kweli wa maendeleo ambayo imekuwa ikishirikiana na Zanzibar katika
kutatua kero zinazoikabili ikiwa ni pamoja na kusaidia wataalamu hasa katika
sekta ya afya.
Naye balozi QiMan
amesema katika kipindi chake cha utumishi hapa nchini, ameshuhudia mafanikio
makubwa yakipatikana yakiwemo kuimarika kwa majengo, huduma za elimu pamoja na
miundombinu ya mawasiliano.
Ameahidi kuwa China
itaendelea kushirikiana na Zanzibar na kutoa michango zaidi katika kusaidia
uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar.
Balozi Chen QiMan amemaliza
muda wa utumishi hapa nchini, baada ya kuitumikia nafasi hiyo ya ubalozi mdogo
kwa kipindi cha miaka miwili na nusu.
0 comments:
Post a Comment