WAKATI Jeshi la Polisi mkoani
Iringa likimkamata na kumshikilia kwa muda wa saa tano kisha kumwachia huru
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe,
pamoja na wabunge watatu, kiongozi huyo amesema kuwa endepo kesi hiyo
itafikishwa mahakamani itakuwa ya 10 kufunguliwa na jeshi hilo.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa
kambi ya upinzani bungeni na vilevile mbunge wa Hai alikamatwa jana asubuhi
pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, Tundu Lissu (Singida Mashariki),
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Diwani
wa Kata ya Mitim
irefu, Frank Nyalusi, wakidaiwa
kuzidisha muda wa mkutano.
Akizungumza na gazeti hili jana,
muda mfupi baada ya kuachiwa alisema kuwa kesi hizo kamwe haziwezi kukiyumbisha
chama hicho na badala yake zimewazidishia mori ya kufanya mageuzi ya kisiasa
nchini ili kuondoa minyororo ya ukiukwaji wa haki.
Alisema kuwa amekuwa akikamatwa
na kufunguliwa kesi za ajabuajabu na jeshi la polisi katika maeneo mbalimbali
nchini wakati akifanya operesheni za kueneza chama mikoani.
Naye Lissu alizungumzia tukio
hilo la kukamatwa kwao akisema limefanyika kisiasa kwa maagizo ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) baada ya kamanda wa polisi kuagizwa na wakuu wa mkoa na wilaya.
Lissu alifafanua kuwa kisheria
hakuna kosa la jinai kama hilo kwa wao kupitisha muda wa mkutano na kwamba
endapo kulikuwa na uvunjifu wa sheria walipaswa kukamatwa siku ileile
walipotelemka jukwaani.
“Hapa hakuna kosa ni siasa tu za
kuelekezwa na CCM halafu polisi wanafuata maelekezo tu.
“Hata maelezo waliyotuandikisha
hawaonyeshi kifungu chochote cha sheria tulichovunja.
“Sheria ya vyama kutozidisha muda
iko kwenye masuala ya mikutano ya uchaguzi, huu si mkutano wa uchaguzi,”
alisema.
Akizungumzia kukamatwa kwa
viongozi hao, kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, alisema kuwa
walizidisha muda wa mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika viwanja vya
Mwembetogwa kwa zaidi ya dakika 25.
“Kutokana na kitendo hicho
tumewashikilia na kuwahoji na wakithibitika kutenda makosa hayo jeshi la polisi
litawafikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema.
Alisema kitendo cha kuzidisha
muda ni kinyume cha sheria na kwamba CHADEMA waliomba kibali cha kufanya
mikutano mitatu mkoani hapa, ratiba yao ilielekeza kuwa wangefika wilaya
Mufindi na kuanza mkutano saa 4:00 hadi 6:00 lakini wakafika saa 9:20 alasiri.
Mungi aliongeza kuwa hata mkutano
wa wilayani Kilolo waliotakiwa kuhutubia saa 6:00 hadi 8:00 mchana wao walifika
saa 4:45 na kuhutubia hadi saa 11:20.
Alisema kuwa Iringa mjini
waliomba kuanza mkutano wao saa 8:00 mchana lakini wakaanza saa 9:00 alasiri
kumaliza saa 12:25 jioni zikiwa ni dakika 25 zaidi ya muda, kitendo alichokiita
ni uvunjwaji wa sheria za nchi.
Katika mkutano huo uliofanyika
juzi katika viwanja vya Mwembetogwa, Mbowe kabla ya kuanza kuhutubia alilitaka
radhi jeshi la polisi kwa kuchelewa kuanza kwa mkutano huo na mara baada ya
kumaliza aliomba tena radhi.
“Nalishukuru sana jeshi la polisi
kwa kuonyesha ustaarabu kwa kuwa niliwaomba radhi kwa kuchelewa kuanza na
naomba dakika 10 nyingine niweze kumalizia jambo muhimu sana kuhusu mchakato
huu wa rasimu ya Katiba,” alisema Mbowe na kuwataka wananchi waliohudhuria
mkutano huo kuwapigia makofi polisi.
Awali akiwa wilayani Kilolo,
Mbowe alisema kuwa suala la serikali tatu halikwepeki kwani ndilo litaweka
utaratibu mzuri wa kunufaika na rasilimali za taifa kwa pande zote mbili za
Zanzibar na Tanganyika.
Aliwataka wananchi kuacha tofauti
zao za kisiasa ili kuweza kujadili mambo yaliyo muhumu katika rasimu ya katiba.
Mbowe aliongeza kuwa majadiliano
ya rasimu ya katiba mpya hayapaswi kufanyika kwa kificho kwa kuwa ni mali ya
Watanzania wote.
“Tunapozungumza suala la Katiba
ya nchi yetu tuache dini na tofauti zetu pembeni ili tuweze kutengeneza Katiba
nzuri. Wananchi wanapaswa kushirikishwa,” alisema.
Alisema katika taifa kumekuwa na
mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa wananchi ambao unasababishwa na baadhi ya watu
kujigeuza kuwa miungu watu.
“Tunataka kila mmoja awe na haki
ya kumiliki ardhi badala ya watu wachahe kuhodhi kila kitu. Tumeona kuna watu
wachache wanataka kutengeneza Katiba inayowalinda wao. Tunapozungumzia utawala
hatumzungumzi Kikwete bali tunataka kuweka utawala ambao kila mtu atakayeingia
madarakani aweze kufuata taratibu hizo,” alisema.
Kwa Katiba tuliyo nayo leo
tunaweza kuwa na Rais chizi akaipeleka nchi kichizi hivyo hivyo na itabidi
tukubali tu.
Alisema Katiba mpya itaweza
kuwabana wabunge watakaochaguliwa ili waweze kurudi kuwatumikia wananchi wao
badala ya kuhamia na kuishi Dar es Salaam.
“Watawala wetu siku hizi wanafanya mambo ya
siri. Wanasaini mikataba ya siri, wanauza madini na gesi kwa siri na kufanya
nchi kama ni mali yao. Katiba mpya itayamaliza mambo ya siri na kila mmoja
atajua kinachoendelea,” alisema. TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Post a Comment