Tanzania imeichaguliwa na Japan kuwa kitovu cha
biashara na uwekezaji barani Afrika, ili kuiwezesha kuwa na uchumi imara na
wenye uwezo kuondoa umaskini na kuongeza fursa za ajira.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jijini Dar es
Salaam jana, ilisema katika kufikia azma hiyo, Japan itasaidia kuboresha reli
ya kati, kuipanua bandari ya Dar es Salaam iwe ya kisasa na kujenga viwanda
vikiwamo vya kutengeneza pikipiki za Honda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania itapata
fursa ya kuwa mshirika wa kwanza wa Japan, ikiwa ni matokeo ya mazungumzo baina
ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe yaliyofanyika Tokyo
Juni, mwaka huu.
Uamuzi huo wa Japan, ulitangazwa rasmi jana
Ikulu jijini Dar es Salaam na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi
hiyo, Toshimistu Motegi, alipozungumza na Rais Kikwete.
Motegi, alisema Japan itawatumia wataalamu wake
kuiboresha reli ya kati kwa kujenga njia ya kimataifa itakayokuwa mbadala wa
reli nyembamba iliyopo sasa.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, Viwanda na
Biashara, Dk. Abdallah Kigoda na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Motegi ameambatana na wafanyabiashara wa Japan
watakaokutana na wale wa ndani, ikiwa ni moja ya mkakati wa kuifanya Tanzania
nchi ya mfano katika Afrika kwenye uwekezaji na uchumi ulioimarika.
Waziri huyo pia alisema Japan imekusudia
kuhakikisha bidhaa ambazo zinanunuliwa kutoka Japan, zinazalishwa hapa nchini
kwenye viwanda vitakavyojengwa na kampuni za nchini humo.
Alisema, kampuni mbili za Honda na Panasonic
zitajenga viwanda vya kutengeneza pikipiki za Honda na kuzalisha vifaa vya
umeme.
Pia, alisema kadhalika kampuni za Japan
zitawekeza kwenye kilimo hasa cha pamba na kuanzisha viwanda vya nguo.
Akiwa Tokyo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Mkuu,
Abe kuwekeza zaidi barani Afrika akisisitiza kuwa Japan ni moja ya mataifa
makubwa duniani ambayo yamefanikiwa kupata soko Afrika hasa eneo la magari.
0 comments:
Post a Comment