Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe,
amehoji kesi 36 zinazohusiana na dawa za kulevya ambazo Jeshi la Polisi limekaa
kimya kwa kutoeleza hatua zilipofikia, hali ambayo inatia shaka na kudhoofisha
vita dhidi ya biashara hiyo haramu.
Alisema hayo juzi wakati akihojiwa na
televisheni ya Channel Ten kuhusu serikali imejipanga vipi kukabiliana na
biashara ya dawa za kulevya ambayo inaonekana kukithiri nchini na kuathiri
asilimia kubwa ya vijana.
Dk. Mwakyembe alisema ili Watanzania wafahamu
nini kinachoendelea kuhusiana na kesi hizo, ameahidi kuzifuatilia ikiwa ni
mkakati wa kukabiliana na biashara hiyo.
“Nitazifuatilia hizo kesi kwa kumshirikisha
waziri mwenzangu (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ili tujue hizo kesi
zimefikia wapi na pia je, tule (ile) tumifuko (mifuko) twa (ya) dawa za kulevya
zimewekwa wapi? Tusije tukakuta kuna mchanga ndani yake,” alisema Dk.
Mwakyembe.
Kuhusu baadhi ya vigogo kudaiwa kujihusisha na
biashara hiyo, alisema kama yupo mtu ambaye anawafahamu kwa majina vigogo hao
ampelekee taarifa kwani suala hili lilipofikia sasa halihitaji usiri.
Dk. Mwakyembe alisema wizara yake itawasiliana
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili balozi za Tanzania
zilizopo nje, zianze kubana watu wanaojihusisha na biashara hiyo.
Kuhusu maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA), waliodaiwa kula njama za kusafirisha dawa za kulevya
kilo 150 zilizokamatwa nchini Afrika Kusini, alisema atashangaa iwapo atasikia
kuwa wamepeleleza na ushahidi haujajitosheleza.
Alisema baada ya kuweka udhibiti katika viwanja
vya ndege ambavyo vinatumiwa kuingiza na kusafirisha dawa za kulevya nchini,
hatua inayofuata ni kubaini wanaowatuma watu wanaokamatwa wakisafirisha dawa
hizo.
Alisema baada ya kuweka udhibiti katika viwanja
vya ndege ambavyo vinatumiwa kuingiza na kusafirisha dawa za kulevya hapa
nchini, hatua inayofuata ni kufanya utafiti watu wanaokamatwa wakisafirisha
dawa hizo ni nani anayewatuma.
Dk. Mwakyembe alisema biashara hiyo itaweza
kukoma tu iwapo mipaka yote itadhibitiwa kwa ushirikiano wa vyombo vya dola.
Agosti 15 mwaka huu, Dk. Mwakyembe aliwataja
maofisa usalama wanne wanaodaiwa kuhusika katika njama za kusafirishwa kwa dawa
za kulevya kutaka wafukuzwe kazi na kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya
Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya.
Dk. Mwakyembe aliwataja maofisa usalama hao
watakaofukuzwa kazi na kufunguliwa mashtaka ya jinai chini ya Sheria ya Kuzuia
Dawa za Kulevya kuwa ni Yusufu Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na
Mohamed Kalungwana.
Mbali na maofisa hao, pia aliliagiza Jeshi la
Polisi kumwondoa mara moja katika uwanja huo, askari wake, Koplo Ernest na
kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwenye njama za kupitisha
mabegi sita ya dawa za kulevya, yaliyokamatwa nchini Afrika Kusini.
Pia alisema polisi inapaswa kumsaka Nassoro Said
Mangunga aliyevikwepa vyombo vya dola nchini Afrika Kusini na kutoroka na
mabegi matatu ya dawa hizo.
Dk. Mwakyembe alisema mbeba mizigo katika uwanja
huo, Zahoro Mohamed Seleman, anapaswa kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa
mashtaka ili kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai.
Pia ameiagiza
Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake
waliokuwa zamu siku ya tukio, kwa kuchelewa kuwafikisha kwa mbwa wakati mwafaka
kukagua mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya na hivyo kuliletea Taifa
fedheha kubwa.
Alisema ameamua kuchukua hatua hizo kwa kuwa
tukio hilo siyo la kwanza, bali ni sehemu ya matukio mengi ya upitishaji wa
dawa hizo katika uwanja wa JNIA, ambayo taarifa zake zinaifikia serikali pale
watuhumiwa wanapokamatwa nje ya nchi wakitokea Tanzania.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment