Robert Boaz Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro.
Wakati polisi mkoani Kilimanjaro wakitangaza
kuwashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya bilionea wa madini ya
Tanzanite, Erasto Msuya (43), pia wamesema mauaji hayo ni ya kulipiza kisasi
katika biashara ya madini.
Kauli hiyo ilitolewaa jana na Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
juu ya hatua waliyofikia katika kusaka waliohusika na mauaji hayo ambayo
yalitetemesha miji ya Arusha na Moshi.
Msuya aliuawa saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi
kando ya barabara kuu ya Arusha – Moshi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai karibu
na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Agosti 07, mwaka huu na
kufa papo hapo.
Alifika eneo hilo akiwa peke yake baada ya
kupigiwa simu na watu anaowafahamu kwenda kufanya nao biashara inayohisiwa kuwa
ni ya madini ya Tanzanite.
Jana Kamanda Boaz alisema kwamba watuhumiwa hao
ambao ni wakazi wa mikoa ya Arusha na Manyara, walikamatwa juzi na kufanya
mahojiano na makachero wa Polisi na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma
zinazowakabili.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Sharifu Mohamed
Athuman ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini, Musa Juma Mangu ambaye ni dereva
wa magari ya Shangarai mkoani Arusha na Shwaibu Jumanne Saidi, mkazi wa
Mererani mkoani Manyara.
“Hawa tuliowatia mbaroni walikodishwa na
wafanyabiashara waliokula njama za mauaji haya (hakuwataja wafanyabiashara
hao), lakini tumefanya nao mahojiano na wakati wowote tutawaburuza kortini,”
alisema Kamanda Boaz.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, mauaji ya kikatili
ya mfanyabiashara huyo yalisababishwa na kulipizana kisasi katika biashara ya
madini.
“Inavyoonekana marehemu aliwekewa mtego na
wauaji hao kwa kudai kwamba wana kiasi kikubwa cha madini na iko kama ni kulipizana
kisasi kati yao ingawa tumewakamata watuhumiwa watatu,” alifafanua Kamanda
huyo
Boaz alisema katika uchunguzi huo, wamefanikiwa kukamata pikipiki aina
Toyo yenye namba za usajili T 316 CLV, ambayo ilitumika katika mauaji hayo ya
kinyama.
Alisema uchunguzi zaidi juu ya mauaji hayo
unafanyika na wahusika watafikishwa mahakamani taratibu za kuandaa mashtaka
zitakapokamilika.
NIPASHE lilikuwa gazeti la kwanza kuelezea
chanzo cha mauaji hayo ikiyafananisha na uhalifu unaofanywa na wahalifu wa
kikundi cha mafia ambao huuana katika ama kudhumiana fedha au kulipizana kisasi
katika biashara zao chafu.
Katika habari ambayo NIPASHE iliandika Agosti 9,
mwaka huu yenye kichwa cha habari ‘Mauaji Bilionea Arusha ni biashara ya
kimafia’ iliwanukuu baadhi ya wakazi wa jijini Arusha wakisema kuwa kuna kila
dalili kuwa mauaji hayo ni matokeo ya kuzidiana kete katika biashara zisizo
rasmi.
Habari hiyo pia iliongezewa nguvu na hoja ya
watu wengi kwamba katika biashara ya madini ya Tanzanite usiri na kudhulumiana
vimekuwa ni sehemu ya shughuli hiyo kiasi cha kusababisha visasi na hata
mauaji.
“Wewe fikiria inakuwaje mtu abebe Sh. milioni
100 peke yake aende porini kote kule kufanya biashara.
Yaani anakwenda kununua madini porini, hana
ulinzi, hana risiti hana nini… hapa aliitwa kuwa kuna mzigo kumbe
wamemlengesha,” alisema mkazi mmoja wa Arusha ambaye aliomba kusitiriwa jina
lake.
Aliongeza kuwa:
“Unajua hawa wafanyabiashara bwana wana mambo
yao mengi. Kwa sasa ni vigumu kusema hasa nini kimemtokea, lakini najua kwa
miaka mingi mambo yao mengi ni deal (magendo) tu.
Hata hapa unaona wazi kuwa maswali ni mengi
kuliko majibu.
”
Katika habari hiyo pia NIPASHE ilimnukuu
mkazi wa Kaloleni Arusha anayejishughulisha na biashara ya utalii alisema kuwa
ukiwaita wafanyabiashara wa madini wote hasa wenye vitega uchumi vikubwa jijini
humo na kuwauliza nyaraka za shughuli za madini utashangaa kwa kuwa kila kitu
kinafanyika kama watu wanaohama kesho.
“Si unajua bwana hata Benki Kuu ilikwisha kutoa
maagizo kuwa hakuna malipo yanaozidi Sh. milioni 10 yanalipwa kwa cash
(taslimu)? Sasa kama marehemu alikuwa na Sh. milioni 100 kama inavyoelezwa ina
maana alikuwa anavunja sheria na pia anajihatarishia usalama wake mwenyewe,”
alisema mkazi huyo huku akiomba jina lake lisitajwe kwa kuwa biashara za Arusha
zina siasa zake.
Habari hiyo pia ilizungumza na kijana mmoja
mkazi wa Usa River, Uria Nnko, ambaye amekuwa kwenye shughuli ya madini kwa
kitambo sasa, ambaye alisema kuwa kwa muda mrefu sasa biashara ya Tanzanite
jijini Arusha inategemea sana vijana aliosema “wanapiga mzigo” kutoka mgodi wa
Tanzania One.
nko alisema kwa hali inavyoonyesha marehemu aliitwa kwenda
kununua mzigo wa namna hiyo na kwa kuwa anajua hizo shughuli zipo aliingia
kichwa kichwa kumbe safari hii alikuwa amewekewa mtego na waliomuua na
kumpora.
Biashara hiyo imeelezwa kufanywa kwa mfumo wa uuzaji dawa za kulevya
kama ambazo hufanywa duniani na makundi hatari ya uhalifu kama Mafioso (mafia)
ambayo kila kitu humalizwa papo kwa papo bila nyaraka za kiserikali wala kibenki.
Kauli ya Kamanda Boaz sasa inathibitisha uvumi
huu kwamba mauaji ya Msuya ni ya kulipizana kisasi katika biashara ya
Tanzanite.
Msuya alifikwa na maafa hayo baada ya kudaiwa
kupigiwa simu na watu waliotaka kumuuzia madini na kukubaliana wakutane eneo
hilo.
Erasto alikuwa anamiliki mgodi wa Kalo uliopo
Mererani na pia migodi mingine miwili ya baba yake Kikaango Msuya iliopo block
B Mererani.
Mbali na migodi hiyo, Erasto alikuwa anamiliki
vitegauchumi kadhaa ikiwamo hoteli moja kubwa inayojulikana kwa jina la SG
Resort, iliyopo Sakina, Arusha.
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment