Dk. Emmanuel Nchimbi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchini.
Serikali imetangaza rasmi kuendesha operesheni
kabambe, itakayofanyika kwa kushtukiza wakati wowote kuanzia sasa, kuwaondoa
kwa nguvu nchini wahamiaji haramu waliokaidi agizo la Rais Jakaya Kikwete,
lililowataka kurejea makwao kwa hiari yao ndani ya wiki mbili, kuanzia Julai
29, mwaka huu.
Wahamiaji hao haramu, ambao wamekuwa wakiishi
nchini kinyume cha sheria za nchi na taratibu za Idara ya Uhamiaji, wanatoka
katika nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Agizo hilo lilitolewa na Rais Kikwete Julai 29,
mwaka huu, alipofanya ziara katika Mkoa wa Kagera, ambako aliwapa wiki mbili
wahamiaji haramu wawe wamerudi makwao kwa hiari yao, vinginevyo wangekamatwa
katika operesheni maalumu ya kijeshi baada ya muda huo kuisha.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel
Nchimbi, aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana kuwa
operesheni hiyo aliyoiita ya “ghafla”, itafanyika baada ya Rais Kikwete kumpa
kibali cha kuiendesha.
Alisema maeneo yatakayohusika zaidi na
operesheni hiyo ni ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwamba, hawatakuwa na ‘msalie
mtume’ kwa mgeni yeyote atakayebainika kuishi nchini isivyo halali.
“Nimeelekezwa
na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, muda wa kuwaondoa nitakapoona inafaa.
Vyombo
vya dola vitaniambia ni lini. Katika muda huu hatutafanya mzaha na jambo hili.
Hatutavumilia tena wageni haramu,” alisema
Nchimbi.
Aliwataka viongozi wa serikali za vijiji
vilivyoko katika mikoa ya kanda hiyo kufahamu kwamba, ni kosa kisheria kushirikiana
na wahamiaji haramu.
Kutokana na hilo, alionya kuwa watakaobainika
wakiwaficha wahamiaji haramu, watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Awali, Waziri Nchimbi alisema baada ya agizo
hilo la Rais Kikwete, mwitikio umekuwa mzuri na kwamba, hadi kufikia usiku wa
Agosti 18, mwaka huu, wahamiaji haramu 10,672 walikuwa wameondoka nchini na
mali zao.
Alisema kati ya wahamiaji hao haramu, katika
Mkoa wa Kagera, Wanyarwanda walikuwa 6,088, Warundi 4,000 na Waganda 269.
Kwa
mujibu wa Waziri Nchimbi, katika Mkoa wa Kigoma, walioondoka ni 150, kati yao
Warundi ni 142 na DRC ni wanane.
Alisema katika Mkoa wa Geita wahamiaji haramu
walioondoka ni 165; kati yao Wanyarwanda ni 126 na Warundi 39.
Hata hivyo,
alisema kazi ya wahamiaji hao kuondoka nchini, bado inaendelea na kuwataka
wananchi hususan wa Mkoa wa Kagera kuwaacha waondoke bila kunyanyaswa, ikiwamo
kupora mali zao.
Hata hivyo, alisema kati ya wahamiaji haramu walioondoka, 14
wamerudi tena nchini na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha “kichokozi.
”
Alisema Rais Kikwete alitoa agizo lile baada
ya wizara kufanya utafiti na kumpa taarifa na kwamba, wahamiaji haramu
wanaosumbua ni wale wanaomiliki vyeti bandia vya kuzaliwa.
0 comments:
Post a Comment