David Ramadhan, Dar Es Salaam.
Kesi ya Kikatiba dhidi
ya waziri Mkuu Mizengo Pinda, imetajwa rasmi katika Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam,ambapo upande wa walalamikaji wameomba
kupatiwa muda wa siku 14 kupitia pingamizi zilizotolewa na serikali na kisha
kuwasilisha majibu yao.
Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS) wamefungua kesi hiyo ya kikatiba kufuatia kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda bungeni, aliyoitoa katika mkutano wa 11 wa Bunge, kwamba Polisi watatakiwa kuwapiga watu
wanaojihusisha na vurugu.
Kutokana na maombi hayo
ya walalalamikaji LHRC kwa kushirikiana na TLS, mahakama kuu imeahirisha kesi
hiyo hadi Septemba 30 mwaka huu ili waweze kuleta majibu ya pingamizi
zilizotolewa na serikali.
Kesi hiyo namba 24 ya
mwaka 2013, inayosikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji
Kiongozi, Fakihi Jundu, akisaidiana na Dk Fauz Twaib na Augustine Mwarija
imepangwa kusikilizwa pingamizi za awali oktoba 18, mwaka huu baada ya mahakama
hiyo kupokea maelezo toka pande zote za mlalamikaji na mtetezi.
BI. Hellen Kijo Bi Simba
Tambarare Halisi ilipotaka
kuzungumza na jopo la mawakili wa upande wa Serikali wanaomtetea Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, Wakili Nixon Mtimbwa alieleza kuwa hawezi kuzungumza lolote
isipokuwa atafutwe Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika kesi hiyo,
walalamikaji wanadai kuwa kauli
inayodaiwa kutolewa na Waziri Mkuu Pinda
ni kinyume cha katiba kwa kuwa inakiuka Ibara za 12(2) 13(1), 13(3),
13(6)(a-e), hivyo wanaiomba mahakama, itamke wazi kuwa kauli hiyo ni kinyume
cha katiba na imwamuru Waziri Mkuu Mizengo Pinda aifute hadharani kauli yake
hiyo.
Wanadai kuwa kauli na
amri kama hizo zinapotolewa na kiongozi mkubwa na mwenye hadhi kama ya mdaiwa, zinachukuliwa
kama sheria inayopaswa kutekelezwa.
0 comments:
Post a Comment