Mitambo ya IPTL.
Mahakama Kuu ya Tanzania imemwamuru Kabidhi Wasihi kukabidhi
mtambo wa IPTL kwa mmiliki wake mpya ambao ni kampuni ya Pan Africa Power
Solutions Tanzania Limited (PAP), ambayo imeahidi kuongeza uwezo wake hadi
kufikia Megawatts 500.
Jaji John Utamwa alifikia uamuzi huo baada ya
kukubaliana na maombi ya aliyekuwa mbia wa IPTL, kampuni ya VIP Engineering and
Marketing Limited (VIP), kuondoa kesi yake ambayo ilikuwa inalenga kuifilisi
IPTL.
Hapo awali, kulikuwa na wabia wawili ndani ya IPTL ambapo VIP ilikuwa
inamiliki hisa 30 wakati kampuni nyingine ya nje, Mechmar Corporation
(Malaysia) Berhard, ilikuwa ikimiliki hisa 70 asilimia.
Mshauri wa Kimataifa
wa VIP, James Rugemalira, alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa uamuzi wa
kampuni yake kuondoa shauri hilo mahakamani ulitokana na makubaliano na PAP
kuuza hisa zake baada ya Kampuni ya Mechmar kufanya hivyo tangu 2010 na hivyo
kumwezesha mwendeshaji huyo mpya kuzalisha umeme wa uhakika bila vikwazo.
Kufuatia
uamuzi huo, Jaji Utamwa alikubaliana na maombi yote ya VIP kwa vile wadau
wengine katika shauri hilo, yaani IPTL, Mechmar na Kabidhi Wasihi hawakupinga
uamuzi huo.
Kabidhi Wasihi alikuwa alikuwa ameteuliwa na mahakama kushikilia
mitambo ya IPTL akisubiri hatima ya kesi hiyo.
Baadhi ya maombi ya VIP
yaliyokubaliwa kwa mujibu wa uamuzi wa Jaji Utamwa wa Septemba 5, mwaka huu,
mahakama kutengua uteuzi wa Kabidhi Wasihi na kumwamuru amkabidhi mmiliki mpya.
Kwa
mujibu wa maamuzi hayo, PAP imeahidi kulipa madeni yote halali ya IPTL na baada
ya kuongeza uwezo wa mitambo itauza umeme Tanesco kwa gharama nafuu kuliko zote
hapa nchini zinazoanzia dola za kimarekani sita hadi nane kwa kila unit kwa
manufaa ya umma.
Uamuzi wa Jaji Utamwa ulifuatia pia kitendo cha kampuni ya
kisheria ya Law Associates kupitia kwa wakili Gabriel Mnyere, kupiga VIP
kuondoa shauri lake mahakamani kwa madai kuwa ilikuwa haijalipwa haki yake
kufuatia kuiwakilisha katika kesi hiyo mara kadhaa.
Hata hivyo, kitendo hicho
kilipingwa vibaya na jopo la mawakili Michael Ngalo, Respicius Didas and Joseph
Makandege, waliokuwa wanaiwakilisha VIP na IPTL, kwa maelezo kuwa Mahakama haikualikwa
kisawasawa kusikiliza pingamizi hilo kwa vile mwombaji alikosea vifungu vya
sheria na hakuwa na mamlaka ya kuweka zuio hilo.
Jaji Utamwa alikubaliana na
hoja hizo na kubaini mapungufu ya kukosea kifungu sahihi cha kuishawishi
mahakama isikilize pingamizi hilo yalikuwa hayasameheki na hivyo kuyafanya
maombi ya Law Associates yakose mashiko ya kisheria.
Alikubaliana na hoja za
wakili Makandege kuwa sheria ilivyo hivi sasa inapendelea wadau katika shauri
kukaa pamoja na kujaribu kutatua tofauti zao nje ya mahakama.
Jaji Utamwa
alibainisha pia kuwa hata Mahakama ya Rufaa katika maamuzi yake mengi
imeonyesha kuwa wadau katika shauri wana haki ya kufikia makubaliano katika
mashauri ya madai na mahakama lazima iheshimu makubaliano hayo, vinginevyo kama
yanamwelekeo wa kukashifu utaratibu wa kimahakama ama sheria ama manufaa katika
jamii.
Hivyo jaji huyo hakushawishika kwamba makubaliano yaliyofikiwa na wadau
katika kesi ya IPTL yalikuwa na nia ovu na ni kinyume cha sheria, na hivyo mtu
mwingine wa nje katika shauri hilo hawezi kuleta kupinga na kufanya asikilizwe,
vinginevyo kama sheria inampa mamlaka ya kuomba hivyo.
Nipashe.
0 comments:
Post a Comment