Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mnero Wilayani Nachingwea
mkoani Lindi, Andrew Chiunguile, amejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa
kupigwa kwa mawe na magongo na wanafunzi, ambao walimtuhumu kula fedha za
walizolipa kwa ajili ya mitihani ya moko na michango mingine.
Tukio hilo
lilitokea mwishoni mwa wiki majira ya saa 5 asubuhi baada ya wanafunzi
hao kukusanyanyika na kuanza kurusha mawe kwenye majengo ya shule hiyo,
ambayo mengine yalimjeruhi mwalimu huyo.
Afisa Elimu ya Sekondari wa
Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Abdallah Membe, amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo.
Baada ya kuona hali inakuwa mbaya, baadhi ya walimu waliokuwa
shuleni hapo walimchukua mwalimu mwenzao na kumficha kwenye moja ya vyumba vya
shule hiyo hadi askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nachingwea walipofika eneo
hilo.
Membe alisema uongozi wa shule hiyo ulichukua uamuzi wa kuwaita askari
polisi baada ya jitihada ya kuzuia hasira za wanafunzi hao kugonga mwamba
kutokana na kuzidiwa nguvu na wanafunzi hao.
Alisema polisi walifika shuleni
hapo na kuanza kufyatua mabomu ya machozi na ndipo wanafunzi hao walianza
kutawanyika kuondoka kwenye maeneo ya shule.
Membe alisema hasira za wanafunzi
hao zilianza baada ya baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne kuzuiwa
kufanya mtihani wa (moko) kwa madai ya kutolipa ada ya mtihani huo wakati
wenyewe wakisema walishalipa kupitia kwa mwalimu huyo.
Wanafunzi hao
walisema mwalimu huyo alipewa jukumu la kukusanya michango hiyo lakini
hakuziwasilisha fedha hizo kwa mkuu wa sekondari hiyo.
Membe alisema vurugu
hizo zilisababisha mwalimu huyo kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo
na usoni baada ya kupigwa na mawe na magongo.
Alisema vurugu za wanafunzi hao
zimesababisha hasara kubwa kutokana na kuharibu samani mbalimbali
zikiwemo viti, madawati na taa za umeme na kuvujwa kwa milango.
Akizungumzia
malalamiko ya wanafunzi hao, Membe, alisema kuwa ofisi yake inafahamu tatizo
hilo na tayari ilikuwa imepanga siku hiyo ya tukio kukutana nao na kuwapa
ufafanuzi.
Alisema utaratibu ulishafanyika wa kuhakikisha wananfunzi hao
hawaathiriki na upotevu wa fedha hizo kwa kuhakikisha wanafanya mitihani hiyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakanjinga amethibitisha kutokea kwa vurugu
hizo na kusema wanafunzi watatu walishikiliwa kwa muda na jeshi hilo na
kuachiwa baada ya kuchukuliwa maelezo.
Alisema upelelezi unaendelea ili
kubaini chanzo cha vurugu hizo na kuwataka wanafunzi hao kuwa watulivu wakati
serikali inashughulikia malalamiko yao.
0 comments:
Post a Comment