Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimesema Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba hautafika mbali hata kama
wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walitumia uwingi wao bungeni kuupitisha na
kwamba kuendelea kulazimisha suala hilo kunaweza kusababisha machafuko nchini.
Akizungumza
katika mahojiano na kipindi cha NIPASHE, kinachorushwa na Redio One, Mwenyekiti
wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema wabunge wa CCM na viongozi wa
serikali lazima watambue kuwa katiba ni jambo la maridhiano si jambo la
kulazimishana.
“Wabunge wa CCM wanaweza kutunga sheria na muswada wanayotaka
sababu wapo wengi lakini lazima waelewe kwamba kutumia wingi wao kulazimisha
jambo muhimu kama la katiba ni kuweka machafuko ndani ya Taifa,”alisema.
Mbowe
alisema mchakato wa katiba unahitaji hekima na busara sana lakini mambo
yanayofanywa na CCM ni wazi kuwa muswada huo hautafika salama.
“Tunawataka na
tunamuomba Rais na viongozi wengine wa CCM ambao pengine wana hekima kuliko
hata wale waliopo ndani ya bunge watumie fursa hiyo kutafuta namna ya kufikia
mwafaka katika masuala ya katiba,”alisema.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema hivi sasa zipo taarifa kuwa wanaharakati
ambao ni kundi lililopo nje ya wanasiasa wanajipanga kwenda mahakamani kupinga
sheria ya marekebisho ya katiba iliyopitishwa wakati wa mkutano wa 12 wa bunge.
Alisema
Naibu Spika Job Ndugai hakuweza kuheshimu nafasi yake (Mbowe) kama kiongozi wa
kambi ya upinzani bungeni kwa kukataa kumpa nafasi ya kuzungumza jambo ambalo
ni kinyume cha kanuni
“Naibu Spika badala yake aliruhusu askari kuingia bungeni
wakaanza kupiga wabunge, kutumia nguvu ,kutukanwa na mambo ya kudhalilishana,
mnategemea hiyo amani ambayo ingeturudisha bungeni kuendeela na mjadala
ingetoka wapi,”alisema Mbowe.
Mbowe alisema maamuzi ya kutaka muswada huo
ujadiliwe bungeni yalikuwa yamekwisha pitishwa kwenye kikao cha wabunge wa
CCM na kwamba hilo ndilo tatizo la kuwa na viongozi wanatoka chama kimoja
cha siasa.
Kwa upande wake, Naibu Spika, Job Ndugai alisema wabunge wa kambi
ya upinzani walishiriki mjadala wa majadiliano ya Muswada wa Marekebisho ya
Katiba licha ya kuonekana wakitoka nje ya ukumbi wa ubunge kwasababu
walijiandikisha kwenye kitabu cha mahudhurio na kupata posho ya siku hiyo.
0 comments:
Post a Comment