Mjumbe wa Congress ya Marekani, Peter King amesema
magaidi waliovamia jumba la kibiashara la Westgate jijini Nairobi, Kenya
wamepata mafunzo katika nchi yake.
King ambaye anatoka katika chama cha upinzani cha
Republicans amesema kundi hilo pia limewafunza ugaidi baadhi ya Wamarekani
pamoja na Wasomali wanaoishi huko.
Huku hayo yakijiri, Marekani imesema inajipanga
kushambulia vituo kadhaa vya kundi la kigaidi la al-shabab nchini Kenya.
Marekani huenda ikashambulia vituo vingine vya makundi
yenye kufurutu ada barani Afrika.
Hayo yamesemwa na kamanda wa zamani wa jeshi la
Marekani, Peter Chiarelli.
Wakati huo huo, jeshi la Kenya likishirikiana na
vyombo vingine vya usalama vya nchi hiyo, limeendelea na oparesheni kali ya
kujaribu kuwaokoa mateka wanaoshikiliwa na wavamizi hao katika jengo la
Westgate.
Wavamizi hao wanaojumuisha raia wa kigeni kutoka nchi
za Magharibi na Asia na pia raia wa Somalia walivamia jumba hilo lenye maduka
mengi katika mtaa wa kifahari wa Westland siku ya Jumamosi na kuuua makumi ya
watu kwa kuwapiga risasi na hadi sasa bado wanawashikilia mateka watu kadhaa
ambao idadi yao bado haijajulikana.
Waziri wa Usalama wa Taifa nchini Kenya, Joseph Ole
Lenku amewaambia waandishi wa habari kuwa, serikali imedhibiti jengo zima la
Westgate na kwamba magaidi wako katika sehemu moja kwenye ghorofa ya mwisho.
Ole Lenku amewataka wanahabari kuwa makini
wanaporipoti tukio hilo.
Habari za hivi punde zinatupasha kuwa, mmoja wa
magaidi amekamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta
akijaribu kuelekea uturuki.
Hadi tunakwenda hewani bado oparesheni ya kujaribu
kuwakamata magaidi na kuwaokoa mateka ilikuwa ikiendelea.
0 comments:
Post a Comment