Wakati Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)
ikiishauri kuharakisha sera ya gesi badala ya ugawaji wa vitalu, serikali
imeendelea kupuuza ushauri huo na sasa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) imetangaza rasmi kuharakisha suala hilo kwa madai ya kuwahi
ushindani wa masoko ulimwenguni.
TPSF kupitia Mwenyekiti wake, Dk. Reginald
Mengi, na Mkurugenzi Mtendaji wake, Godfrey Simbeye, wiki iliyopita walitoa tamko
la pamoja wakisema kama ugawaji wa vitalu utafanyika Oktoba, mwaka huu, kama
ilivyopangwa, Watanzania hawatakuwa na fursa ya kumiliki rasilimali yao.
Lakini
pamoja na ushauri huo, jana Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael Mwenda,
aliwaambia waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana kuwa kwa sasa hivi
ulimwenguni kuna ushindani wa kuwahi masoko ya gesi.
Hivyo, akasema endapo
kama masoko yatafurika kabla ya kuyawahi, inawezekana kulazimika kuuza gesi kwa
bei ya chini sana ama kushindwa kuendeleza kabisa gesi iliyogunduliwa.
“Mfano
halisi ni gesi ya Songosongo, ambayo siku za nyuma haikuweza kupata soko na
hivyo kubaki ardhini kwa miaka 30 kabla ya kuanza kutumika,” alisema Mwenda.
Kutokana
na hilo, alisema kuongeza hazina za gesi kwa kuendelea kutafuta, kutajenga
imani kwa wawekezaji hasa kwa kuwa mikataba ya gesi huwa inakuwa ya muda mrefu
kutokana na uwekezaji wake, ambao hutumia mitaji mikubwa.
Alisema kwa sasa
Msumbiji wameshaongeza hazina yao ya gesi iliyopo ardhini kufikia takriban 200
TCF wakati hazina ya gesi ya Tanzania iliyopo ardhini ni takriban 43 TCF na
kusema mwekezaji atavutiwa zaidi kuwekeza pale ambako hazina ya gesi ni kubwa.
“Kwa
kuzingatia haya ni muhimu kwa Taifa letu kuendeleza mchakato wa kutoa vitalu
ili shughuli za utafutaji ziendelee na ikiwezekana ugunduzi wa mafuta ufanyike
na au hazina ya gesi iongezeke.
Kuongezeka kwa hazina ya gesi kuvutiwa zaidi
wawekezaji na kutapunguza gharama za utafutaji na uzalishaji siku za baadaye,
”
alisema Mwenda.
Alisema kwa sasa serikali inatarajia kutoa vitalu vingine saba
baharini; pia eneo la Ziwa Tanganyika Kaskazini katika duru ya nne
itakayozinduliwa Oktoba 25, mwaka huu.
Kuhusu ushiriki wa wazawa, Mwenda
alisema wanaweza kushiriki kwa kutoa huduma muhimu na usambazaji wa bidhaa
zinazohitajika na zinazotumika katika utekelezaji wa shughuli za utafutaji na
uchimbaji.
Alisema katika nchi nyingine, wananchi huhusika katika kununua hisa
za kampuni zinazofanya kazi katika masoko ya mitaji kwa kutegemea kama kampuni
itafanya vizuri na kufanya ugunduzi, hivyo hisa za wawekezaji kuongezeka
thamani.
Mwenda alisema uwekezaji katika miradi ya utafutaji wa mafuta na gesi
unahitaji kiasi kikubwa cha fedha huku kukiwa hakuna uhakika wa mrejesho wa
uwekezaji huo.
Alisema kuchimba kisima kimoja katika maeneo ya nchi kavu
inagharimu takriban dola za Marekani milioni 40 (Sh. bilioni 64) na katika
maeneo ya kina kirefu cha bahari kisima kimoja kinagharimu takriban dola za
Marekani milioni 120 (Sh. bilioni 190) na kwamba, kwa kawaida ni lazima visima
kadhaa vichimbwe kabla ya kuanza uzalishaji.
NIPASHE.
0 comments:
Post a Comment