Utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya watoto wa kike
8,000 kila mwaka wanaacha shule kutokana na ndoa za utotoni, mila na
desturi potofu na mazingira hatarishi ya kupata elimu.
Utafiti uliofanywa na
shirika la kutetea haki za watoto la Plan International Tanzania, umebaini kuwa
mfumo dume katika jamii pia unachangia kwa asilimia kubwa katika kuwafanya
watoto wasiendelee na masomo.
Hayo yalielezwa jana na Meneja Ushauri wa
shirika hilo, Jane Mrema, wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kupinga ukatili
wa kijinsia yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema jamii bado inahitaji
kupewa elimu zaidi ili kuondokana na mifumo kandamizi kwa watoto wa kike
inayowapelekea kushindwa kusoma.
“Jamii ikipewa elimu ya kutosha itasaidia
kuondoa vikwazo vinavyopelekea watoto kushindwa kuendelea na shule pia wadau
kusaidia kuboresha mazingira ya shule ili kuwajengea mazingira rafiki,” alisema
Mrema.
Aidha Shirika hilo katika kuhakikisha watoto wa kike na wenye ulemavu
wanaendelea na masomo, limewasaidia watoto 450 kupata elimu ya sekondari
na wengine 400 elimu ya msingi katika mikoa minne nchini.
Mrema alisema,
pia katika juhudi za kuwasaidia watoto hao wamejenga miundombinu rafiki katika
shule, kama vyoo na visima vya maji katika mikoa ya Mwanza, Morogoro na Pwani.
0 comments:
Post a Comment