Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM),
huku jumuiya hiyo ikitengua uteuzi wa wakuu watatu wa idara zake ambao
walikataliwa na Baraza Kuu la chombo hicho lililokutana hivi karibuni, Visiwani
Zanzibar.
Wakati hayo yakiendelea kuna na taarifa kwamba kumekuwa na
mwendelezo wa harakati za kuandaa mkakati wa kumwondoa madarakani mwenyekiti wa
jumuiya hiyo, Sadifa Juma Khamis na kwamba vikao vya kupanga mkakati huo
vilianza mara tu baada ya mkutano wa Zanzibar.
Watendaji waliosimamishwa ni
Wakuu wa Idara za Oganaizesheni, Tumaini Mwakasege, Fedha na Uchumi, Omary
Suleiman na yule wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Omary Justus.
Katibu
Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda alilithibitishia gazeti hili kung’olewa kwa watendaji
hao na kwamba kuendelea kwao na majukumu yao kutategemea iwapo watathibitishwa
na Baraza Kuu la jumuiya hiyo linalokutana mjini Dodoma Oktoba mwaka huu.
“Sisi
tuliomba hawa wathibitishwe kwenye kikao kijacho kwa kuwa kulitokea kidogo
mkanganyiko wajumbe wakataka tujadili suala hili kwenye Baraza Kuu lililopita
lakini kwa kuwa tulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu tukaomba
suala hili lisogezwe mbele,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari watendaji
hao walikuwa wameanza kazi lakini kutokana na baadhi ya kanuni kujikanganya,
wameona ni vyema waache suala hilo mpaka kwenye mkutano ujao.
“Kuna kanuni
inayotoa mamlaka kwa Kamati ya Utekelezaji na vilevile Baraza Kuu, kwa hiyo
inabidi sasa tuweke kwanza mambo sawa kisha kwenye Baraza Kuu la Oktoba, hawa
watathibishwa,” alisema.
Hata hivyo habari ambazo zimelifikia gazeti hili
zinasema si rahisi kwa wakuu hao wa idara kurejea kwenye nafasi zao, kwani
kitendo cha wajumbe kuwakataa katika kikao cha Zanzibar kinathibitisha kwamba
hawana imani nao.
“Kama wajumbe wa Baraza Kuu wangekuwa wanawaamini, shinikizo
lingekuwa ni kuwathibitisha, lakini sisi wajumbe ni kwamba hatuwataki.
Inabidi
Sadifa na kamati yake ya utekelezaji watuteulie watu wengine,” alisema mmoja wa
viongozi wa UVCCM wa mikoa ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Suala la uteuzi
wa wakuu wa idara za UVCCM pia ni mtihani wa kwanza kwa Katibu Mkuu mpya,
Mapunda ambaye mara baada ya kuthibitishwa alionja chungu ya mgogoro katika
taasisi ambayo yeye ni mtendaji mkuu wake, pale alipopingwa vikali na wajumbe,
alipojaribu kumtetea Sadifa.
Katika mazingira hayo, Mapunda anaweza kujikuta
katika mgogoro mkubwa zaidi na wajumbe wa Baraza Kuu, ikiwa atawasilisha majina
ya watu walewale waliong’olewa ili wapigiwe kura kwa ajili ya kuthibitishwa.Vikao
vya Siri.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment