Wanafunzi
wawili wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari matombo katika wilaya ya
morogoro wamejeruhiwa, na wengine watatu kunusurika, baada ya kulipukiwa na
kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu, wakati wakitoka shuleni.
Wanafunzi
hao waliojeruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao ni Luciani Juma
(14) na Anthonia Charles (15), wakazi wa kijiji cha Konde, Tarafa ya Matombo
wilayani Morogoro, ambapo Luciani aliyelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa
wa Morogoro kwa matibabu, amesema kuwa walipatwa na tukio hilo wakati wakitokea
shuleni, ambapo njiani walikutana na kitu mfano wa balbu ya tochi ambacho
hata asubuhi wakati wa kwenda shule walikiona na kukipuuza, na mmoja
wawanafunzi alikirushia ganda la muwa aliokuwa akila, na kililipuka na kutoa
mshindo mkubwa.
Daktari
anayemtibu Lucien katika wadi namba moja ya hospitali ya rufaa ya mkoa wa
Morogoro, aliyejulikana kwa jina moja Dk. Francis amesema majeruhi huyo
anaendelea vizuri, na amepata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake
ikiwemo sehemu za siri, kwenye paja na sehemu ya nyonga na kwamba katika maeneo
hayo walifanikiwa kutoa vitu mfano wa chuma.
Kaimu
kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro John Laswai, amethibitisha kujeruhiwa kwa
wanafunzi hao, ambapo majeruhi Anthonia ametibiwa na kuruhusiwa na kwamba
polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kubaini kitu kilichowajeruhi wanafunzi
hao, ambacho kilitoa mshindo mkubwa na mtawanyiko wa vyuma, kama kilikuwa ni
bomu ama vinginevyo.
0 comments:
Post a Comment