Watu sita wamefariki dunia na wengine 34 kujeruhiwa katika
ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Chinangali wilayani Chamwino mkoani
Dodoma baada ya basi la kampuni ya Al Sayeed lililokuwa likitokea jijini
Dar-Es-Salaam kwenda Dodoma kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililobeba
shehena ya mahindi likitokea Dodoma kwenda Dar es salaam.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo kaimu kamanda wa polisi
mkoa wa Dodoma Mrakibu Mwandamizi Damas Nyanda amesema chanzo cha ajali hiyo ni
mwendo kasi wa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T 433 BLR aina ya
Youtong ambaye alishindwa kulimudu na kuacha njia na kulivaa lori aina ya
Layland Daf lenye namba za usajili T 102 CGR likiwa na tela lenye namba za T
928 na kusababisha watu watano kufariki papo hapo.
Kwa upande wa baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamelalamikia
uhaba wa vyombo vya uokoaji ambapo wamesema kama vyombo vya uokoaji vingefika
kwa wakati huenda watu wote wanne waliofariki kwenye lori wangeokolewa.
Nao baadhi ya majeruhi waliolazwa katika hosipitali ya rufaa
ya Dodoma wamesema kabla ya kutokea kwa ajali hiyo dereva wa basi hilo alikuwa
katika mwendo kasi na baada ya kuliona lori hilo alifunga breki za ghafla na
kusababisha basi hilo kulivaa lori hilo huku mganga mfawidhi wa hosipitali hiyo
Dk Mzee Nasoro akasema walipokea majeruhi 20 na mmoja kati yao amefariki dunia.
0 comments:
Post a Comment